36. Njia mbalimbali za kufunga swawm ya ´Aashuuraa´

Wanachuoni wametaja ya kuwa daraja bora zaidi ya kufunga siku ya ´Aashuuraa´ ni kufunga siku tatu: siku ya tisa, kumi na kumi na moja. Wamejengea hoja kwa dalili ya Hadiyth ya Ibn ´Abbaas:

“Jitofautisheni na mayahudi na fungeni siku kabla yake na baada yake.”

Ingawa Hadiyth hii ni dhaifu na haitegemezwi isipokuwa kusemwa kuwa kufunga hizo siku tatu kunaongezea fadhilah juu ya ´Aashuuraa kwa kuwa ni ndani ya mwezi mtukufu na kumekuja himizo la kuufunga mwezi huo, na pia hupatikana fadhilah ya kufunga siku tatu kila mwezi. Imepokelewa kutoka kwa Imaam Ahmad ya kuwa amesema:

“Anayetaka kufunga ´Aashuuraa´ basi afunge tarehe tisa na kumi; isipokuwa ikiwa haelewi tarehe sahihi basi afunge siku tatu.” Ibn Siryin anaonelea hivo.”[1]

Daraja ya pili ni kufunga siku ya tarehe tisa na ya kumi, kama ilivyokuja katika Hadiyth nyingi zilizotangulia.

Daraja ya tatu ni kufunga tarehe ya tisa na tarehe ya kumi au ya kumi na moja kwa kutegemea Hadiyth dhaifu ya Ibn ´Abbaas kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fungeni siku ya ´Aashuuraa´ na nendeni kinyume na mayahudi kwa kufunga kabla yake au baada yake.”[2]

Daraja ya nne ni kufunga siku ya tarehe kumi peke yake ambapo baadhi ya wanazuoni wamechukia kwa kuwa ni kujifananisha na watu wa Kitabu, kama ilivyo mashuhuri kutoka kwa Ibn ´Abbaas na pia ni madhehebu ya Imaam Ahmad na baadhi ya Hanafiyyah, huku wengine wakisema kuwa haichukizwi kwa sababu ni siku yenye fadhilah. Hivyo inapendelewa kuifunga ili kupata thawabu zake. Dhahiri ni kwamba kufunga siku ya kumi pekee inachukiza kwa mwenye uwezo wa kuambatanisha siku nyingine nayo, lakini haifuti kupata thawabu kwa mwenye kuifunga pekee kwani atalipwa – Allaah akitaka.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, jamaa zake na Mawahabah wote.

[1] al-Mughniy (4/441) na ”Iqtidhwaa´-us-Swiraatw al-Mustaqiym” (1/419).

[2] Ameipokea Ahmad (4/52), Ibn Khuzaymah (3/290) na (2095), at-Twahaawiy  katika “Sharh Ma´aaniy al-Aathaar” (2/78) na al-Bayhaqiy (4/287) kupitia njia ya Muhammad bin ´Abdir-Rahman bin Abiy Laylaa, kutoka kwa Daawuud bin ´Aliy, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake Ibn ´Abbaas kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mlolongo wake wa wapokezi ni dhaifu na haisihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 64-65
  • Imechapishwa: 20/05/2025