Yule mtu ambaye haridhiki mpaka afikie katika ngazi ya kuwahukumu watu, kwa njia ya kwamba watu wa sasa hawamuadhimishi wala kumtambua mtu isipokuwa aliyeko hivo, basi hakika amebadilisha yaliyo duni kwa yaliyo bora na ametoka katika ngazi ya wanazuoni na kwenda katika ngazi ya madhalimu. Kwa ajili hiyo wamesema baadhi ya Salaf walipotaka kupewa kazi ya ukadhi wakakataa:

“Nimejifunza elimu ili nifufuliwe pamoja na Mitume, na si pamoja na wafalme. Wanazuoni watafufuliwa pamoja na Mitume na mahakimu watafufuliwa pamoja na wafalme.”

Ni lazima kwa muumini awe na subira kidogo ili aweze kufikia katika mapumziko marefu. Akikata tamaa na asifanye subira, basi yeye ni kama alivosema Ibn-ul-Mubaarak:

“Mwenye kusubiri, husubiria kidogo, na mwenye kukata tamaa, hustareheka kidogo.”

Imaam ash-Shaafi´iy amesema:

Ee nafsi! Si venginevyo isipokuwa ni subira tu ya masiku machache;

kana kwamba muda wake ni mkorogano wa ndoto

Ee nafsi! Hakikisha ni mwenye kupita duniani kwa upesi

na uachane nayo – kwani hakika maisha yako huko mbele

Tunamuomba Allaah (Ta´ala) elimu yenye manufaa na tunajilinda Kwake dhidi ya elimu isiyokuwa na manufaa, dhidi ya moyo usionyenyekea, dhidi ya nafsi isiyoshiba na dhidi ya du´aa isiyoitikiwa. Ee Allaah! Hakika sisi tunaomba kinga Kwako kutokamana na mambo haya manne. Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na amani zimwendee bwana wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 90-91
  • Imechapishwa: 04/10/2021