Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

19 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akipaka wanja ilihali amefunga katika Ramadhaan.”[1]

Ameipokea Ibn Maajah kwa cheni ya wapokezi nyonge. at-Tirmidhiy amesema:

“Hakukusihi kitu juu ya maudhui haya.”

MAELEZO

Wanazuoni wametofautiana kuhusu hukumu mfungaji kupaka wanja kwa mitazamo miwili:

1 – Mtu anayefunga amekatazwa kutumia wanja na kwamba inabatilisha swawm. Hayo ndio maoni ya Imaam Ahmad na yamepokelewa na at-Tirmidhiy kutoka kwa Sufyaan, kutoka kwa Ibn-ul-Mubaarak na kutoka kwa Ishaaq[2]. Wamejengea hoja kwa yale aliyopokea Abu Daawuud kupitia kwa ´Abdur-Rahmaan bin an-Nu’man bin Ma’bad bin Huwdah, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa aliagiza kutumia Ithmid yenye harufu nzuri wakati wa kulala na akasema:

“Ajiepushe nayo mfungaji.”[3]

Pia wametumia hoja kwamba jicho ni njia ya kuingiza kitu mwilini. Dalili ya hilo ni kwamba mtu anaweza kuhisi ladha ya wanja kooni mwake.

2 – Inaruhusiwa kwa mwenye kufunga kujipaka wanja na kwamba haibatilishi swawm. Ni mamoja anahisi ladha yake kooni au hahisi. Hayo ni maoni ya Hanafiyyah na Shaafi´iyyah. Aidha ndio maoni yaliyopewa nguvu na Shaykh-ul Islaam Ibn Taymiyyah[4]. Wamejengea hoja kwa Hadiyth ya mlango huu na kwamba jicho si njia ya kuingiza chakula au kinywaji. Kwa hivyo hakuharibu swawm.

Haya ya pili ndio maoni yenye nguvu zaidi, kwa sababu hakukuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) chochote juu ya hilo. Msingi ni kusihi kwa funga, isipokuwa kama kuna dalili sahihi na wazi inayofahamisha kinyume chake. Wanja haufunguzi, hata kama mtu atahisi ladha yake kooni. Kwa sababu si chakula, si kinywaji na wala si kitu chenye maana ya chakula au kinywaji. Jengine ni kwamba jicho si njia ya kupitisha chakula na kinywaji.

Aidha wanja ni jambo linalohitajika mara kwa mara na watu. Kwa maana nyingine lau kama lingekuwa linabatilisha swawm, basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angelibainisha wazi kama alivyobainisha mambo mengine yanayobatilisha swawm. Kwa kuwa hakufanya hivyo, hii ni dalili kwamba kutumia wanja hakuharibu swawm.

Jengine ni kwamba Abu Daawuud amepokea kwa cheni yake ya wapokezi kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba alikuwa akitumia wanja hali ya kuwa amefunga. Pia Abu Daawuud amepokea kupitia kwa al-A‘mash ambaye ameeleza:

“Sijawahi kuona yeyote miongoni mwa wenzetu akichukia wanja kwa mfungaji. Isitoshe Ibraahiym (yaani an-Nakha‘iy) alikuwa akimruhusu mfungaji kutumia dawa ya jicho.”

an-Nawawiy amenakili kwamba Ibn-ul-Mundhiriy amepokea maoni haya kutoka kwa ‘Atwaa’, al-Hasan al-Baswriy, an-Nakha‘iy na al-Awzaa‘iy. Wengine wameyapokea kutoka kwa Ibn ‘Abbaas, Anas na Ibn Abiy Awfaa (Radhiya Allaahu ´anhum) na akamuegemezea nayo Daawuud adh-Dhwaahiriy.

[1] Ibn Maajah (1678).

[2] al-Mughniy (04/353).

[3] as-Sunan (2377).

[4] al-Hidaayah (01/126), al-Majmuu´” (06/348), “Haqiyqat-us-Swiyaam”, uk. 37.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/47-49)
  • Imechapishwa: 24/02/2025