al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

”Swawm ni kinga. Ikiwa ni siku ya swawm ya mmoja wenu, basi asiseme maneno machafu wala asitende ujinga. Ikiwa mtu atapigana naye au atamtukana, basi aseme: ”Mimi ni mwenye kufunga.”[1]

Maana ya kinga ni kitu kinachomfunika mwenyewe na kumzuia asipatwe na madhara ya mwingine. Hivyo swawm humhifadhi mwenyewe dhidi ya kuangukia katika maasi ambayo adhabu yake ni adhabu ya haraka duniani na ya Aakhirah.

Maneno machafu ni ufidhuli na maneno mabaya. Ahmad na wengine wamepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

”Swawm ni kinga muda wa kuwa haijavunjwa.” Akaulizwa: ”Inavunjwa vipi?” Akasema: ”Kwa kusema uwongo au kusengenya.”[2]

Katika haya kuna dalili kwamba kusengenya kunaiharibu na kuiathiri swawm. Kinga ikichanika haimnufaishi kitu mwenyewe. Vivyo hivyo funga ikiharibika haimnufaishi kitu mwenye kufunga.

Usengenyi, kama alivyobainisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Kumtaja ndugu yako kwa jambo analolichukia.”[3]

[1] al-Bukhaariy (1894) na Muslim (1151).

[2] Sehemu yake ya kwanza imepokelewa na an-Nasaa´iy (04/167) (nr. 2231), Ahmad (01/195) (nr. 196), Abu Ya’laa (02/181) (nr. 878), al-Bayhaqiy (07/173) (nr. 3294), (07/249) (nr. 3370)).

[3] Muslim (2589), Abu Daawuud (4874) na at-Tirmidhiy (1934).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tawjiyhaat wa Tanbiyhaat lil-Fataati al-Muslimah, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 28/02/2026