35. Hadiyth ”Mtume alipoifunga siku ya ´Aashuuraa’… ”

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza ya kwamba:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoifunga siku ya ´Aashuuraa’ na kuwaamrisha watu kuifunga, wakamwambia: “Ee Mtume wa Allaah, hii ni siku inayotukuzwa na mayahudi na manaswara.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Basi mwaka ujao – Allaah akitaka – tutafunga pia siku ya tisa.” Akasema: ”Haikufika mwaka ujao hadi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafariki.”

Ameipokea Muslim.

Imekuja katika upokezi wa Muslim:

“Kwa hakika nikibakia hadi mwaka ujao, basi nitafunga siku ya tisa.”[1]

MAELEZO

Hadiyth hii ni dalili kuwa inapendekezwa kwa anayetaka kufunga siku ya ´Aashuuraa’ afunge pia siku ya tisa kabla yake – ambayo ni siku ya tarehe ya tisa – ili kuambatana na siku ya kumi. Hii ni Sunnah japokuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakufunga siku hiyo, kwani alidhamiria kuifunga. Lengo – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ni kuifunga pamoja na siku ya kumi ili kwenda kinyume na watu wa Kitabu, kwa sababu wao walikuwa wanafunga siku ya kumi peke yake. Hili linaashiriwa katika baadhi ya masimulizi ndani ya Muslim. Imesihi ya kwamba Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fungeni siku ya tisa na kumi; nendeni kinyume na mayahudi.”[2]

Katika hili kuna dalili wazi kabisa ya kwamba muislamu amekatazwa kujifananisha na makafiri na watu wa Kitabu, kwani kujifananisha nao kuna manufaa makubwa na faida nyingi. Miongoni mwayo ni:

1 – Kukata njia zinazopelekea kuwapenda na kuwafuata.

2 – Kuonyesha kujitenga nao kwa ajili ya Allaah.

3 – Kuwachukia kwa ajili ya Allaah.

4 – Waislamu kuonyesha upekee na kujipambanua.

[1] Muslim (1134).

[2] ´Abdur-Razzaaq (4/287), at-Twahaawiy (2/78) na al-Bayhaqiy (4/278) kutoka kwa Jurayj, kutoka kwa ´Atwaa´, kutoka kwa Ibn ´Abbaas kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 63-64
  • Imechapishwa: 20/05/2025