34. Ndio maana Ahl-ul-Bid´ah wanawapachika Ahl-us-Sunnah majina ya bandia

Watu wa matamanio, wazushi na wenye kwenda kinyume wamewazulia Ahl-us-Sunnah majina ya bandia na mabaya. Malengo yao ni kuwaponda, kuwatukana na kuwakejeli mbele ya wapumbavu na wajinga.

Murji-ah wanawaita Ahl-us-Sunnah “Shukkaak”, wenye mashaka. Murji-ah wamesema uwongo. Kama kuna yeyote mwenye mashaka na kukadhibisha basi ni wao.

Qadariyyah wanawaita Ahl-us-Sunnah wanaothibitisha “Jabriyyah”. Qadariyyah wamesema uwongo. Uwongo na kwenda kinyume kunaendana na wao zaidi. Wanakanusha uwezo wa Allaah juu ya viumbe Wake. Wanamnasibishia (Subhaanah) kwa njia isiyostahiki.

Jahmiyyah wanawaita Ahl-us-Sunnah “Mushabbihah”. Jahmiyyah, maadui wa Allaah, wamesema uwongo. Kufananisha na kukadhibisha kunaendana na wao zaidi. Wamemzulia uzushi na uwongo Allaah (´Azza wa Jall) na wamekufuru kwa ´Aqiydah yao.

Raafidhwah wanawaita Ahl-us-Sunnah “Naaswibah”.  Raafidhwah wamesema uwongo. Jina hilo linaendana na wao zaidi kwa sababu wanawatukana Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwasemea uwongo. Wanawatuhumu kutokuwa waadilifu kwa dhuluma, uwongo kabisa, ujasiri wa kipumbavu kwa Allaah (´Azza wa Jall) na kupunguza haki ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Naapa kwa jina la Allaah kukejeliwa na kulipizwa kisasi kunaendana zaidi na wao.

Khawaarij wanawaita Ahl-us-Sunnah “Murji-ah.” Khawaarij wamesema uwongo. Bali wao ndio Murji-ah kwa sababu wanaona wao pekee ndio waumini na wenye haki na wengine wote ni makafiri.

Watu wa maoni wanawaita Ahl-us-Sunnah “Naabitah” na “Hashwiyyah”. Watu wa maoni, maadui wa Allaah, wamesema uwongo. Bali wao ndio Naabitah na Hashwiyyah. Wameacha mapokezi na Hadiyth zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wametendea kazi maoni yao wenyewe, wameilinganisha dini kwa mitazamo ya kibinafsi wanayoona kuwa mizuri na wamehukumu kwa yanayopingana na Qur-aan na Sunnah. Wao ndio Ahl-ul-Bid´ah, wajinga na wapotevu ambao wanajipinda kuitafuta dunia kwa uwongo na uzushi.

  • Mhusika: Imaam Harb bin Ismaa´iyl al-Kirmaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-us-Sunnah, uk. 96-100
  • Imechapishwa: 08/06/2022