Hadiyth ya Shaddaad bin Aws ni dalili kwamba kuumikwa kunaharibu swawm, kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Amefungua mwenye kuumika na mwenye kuumikwa.”
Hii ni kwa sababu mfungaji anayefanyiwa chuku swawm yake inaharibika kwa sababu ya kutoka kwa damu, kwani inamfanya awe dhaifu. Ama anyepiga chuku swawm yake inaharibika kwa sababu ya kunyonya damu. Hayo ndio maoni ya Imaaam Ahmad na yakachaguliwa na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na mwanafunzi wake Ibn-ul-Qayyim[1].
Wanahifadhi wakubwa wa Hadiyth wameikosoa Hadiyth ya Ibn ´Abbaas, akiwemo Imaam Ahmad, Ibn-ul-Madiyniy, Yahyaa Ibn Ma’iyn, Yahyaa bin Sa´iyd al-Qattwaan na Abu Haatim[2]. Wamesema sentesi isemayo: ”… ilihali amefunga.” halikuhifadhiwa. Muhannaa amesema:
”Nilimuuliza Ahmad kuhusu Hadiyth hiyo ambapo akasema: ”Ndani yake hakuna ”mfungaji”. Bali kilichomo ni ”… ilihali ni Muhrim”.”[3]
Kinachoonekana – na Allaah anajua zaidi – ni maoni ya jopo la wanazuoni na kwamba kupiga chuku ilikuwa inaharibu swawm mwanzoni, lakini hukumu hiyo ilifutwa baadaye. Dalili ya kufutwa kwa hukumu ni Hadiyth ya Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:
”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliruhusu busu kwa mfungaji na akamruhusu kuumikwa.”[4]
Haafidhw amesema:
“Ibn Hazm amesema kuwa cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh. Kwa hivyo ni lazima tuifuate, kwani ruhusa hutolewa baada ya agizo la Kishari´ah. Ni dalili ya kufutwa kwa hukumu ya kufungua kwa kufanya chuku, ni mamoja iwe kwa mwenye kuumika na mwenye kuumikwa.”[5]
Udhahiri ni kwamba Hadiyth zinazoruhusu chuku zimekuja baadaye kuliko zile Hadiyth zinazokataza. Pia imepokelewa kwa cheni ya wapokezi kama maneno ya Swahabah inayosema:
”Mfungaji ameruhusiwa kupiga chuku na busu.”[6]
Hadiyth hii ina hukumu ya kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa sababu ruhusa katika hukumu za Kishari´ah ni zenye hutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hadiyth hii yenye hukumu ya kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inafasiriwa kwa ujio wa nyingine iliyo wazi. Hivyo inathibitisha kufutwa kwa Hadiyth ya Shaddaad bin Aws (Radhiya Allaahu ´anh) inayoonyesha kuwa kuumikwa kunaharibu swawm. Pia Hadiyth ya Anas inajulisha juu ya hilo, kama tulivyotangulia kueleza.
[1] al-Mughniy (04/350), ”Haqiyqat-us-Swiyaam”, uk. 81 na baada yake, ”Tahdhiyb Mukhtaswar-is-Sunan” (03/242).
[2] Tanqiyh-ut-Tahqiyq (02/325) na ”at-Takhliysw” (02/203).
[3] al-Fataawaa (25/253).
[4] an-Nasaa´iy (03/345), Ibn Khuzaymah (03/230), Ibn Hazm (06/204) na wengineo. Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa´” (04/75)
[5] al-Muhallaa (06/205) na “Fath-ul-Baariy” (04/178).
[6] Ibn Khuzaymah (3/231), ad-Daaraqutwniy (02/182) na al-Bayhaqiy (04/264). Abu Haatim ameyapa nguvu maoni yanayosema kuwa ni maneno ya Swahabah (686), Ibn Khuzaymah na at-Tirmidhiy katika ”al-´Ilal” (01/367) na wengineo.
- Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/45-46)
- Imechapishwa: 19/02/2025
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)