Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

56 – ´Arshi na Kursiy ni haki.

MAELEZO

´Arshi ndio kiumbe kikubwa sana, kama inavofahamisha Qur-aan na Sunnah. Kwa ajili hiyo Allaah akaegemeza Kwake Mwenyewe pale aliposema:

وَهُوَ الْغَفُورُ الْوَدُودُ ذُو الْعَرْشِ الْمَجِيدُ

”Naye ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye upendo wa ndani kabisa, Mwenye ‘Arshi, Tukufu.”[1]

Zipo Aayah zingine ambazo unaweza kuzipata kwenye maelezo ya [Ibn Abiy-´Izz].

Utambulisho wa ´Arshi kilugha ni kiti cha mfalme. Miongoni mwa sifa zake ndani ya Qur-aan:

وَالْمَلَكُ عَلَىٰ أَرْجَائِهَا ۚ وَيَحْمِلُ عَرْشَ رَبِّكَ فَوْقَهُمْ يَوْمَئِذٍ ثَمَانِيَةٌ

”… Malaika watakuwa kandoni mwake na watabeba ‘Arshi ya Mola wako juu yao siku hiyo [Malaika] wanane.”[2]

Iko juu ya maji. Imesihi katika Sunnah ya kwamba umbali uliopo baina ya ncha ya masikio ya wabeba ´Arshi na shingo zao ni sawa na ndege kuruka kwa miaka 700, kwamba iko na miguu na kwamba ndio paa la Pepo ya Firdaws. Yote hayo yametajwa katika maelezo ya [Ibn Abiy-´Izz]. Yote hayo yanabatilisha kuipindisha ´Arshi maana ya kwamba ni ibara ya ufalme na utawala.

Kuhusu Kursiy, Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ

”Wala hawakizunguki chochote katika elimu Yake isipokuwa kwa akitakacho. Kursiy Yake imeenea mbingu na ardhi.”[3]

Kursiy ni ile inayokuwa mbele ya ´Arshi. Imesihi kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesema:

”Kursiy ni mahali pa kuwekea miguu miwili, na ´Arshi hakuna awezaye kuikadiria isipokuwa Allaah pekee.”[4]

Nimeikagua katika kitabu changu ”Mukhtaswar-ul-´Uluww” (36).

Hakuna kilichosihi juu ya Kursiy isipokuwa maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mbingu saba na ardhi saba ukizilinganisha na Kursiy ni kama mfano wa pete iliyotupwa kwenye jangwa. Na tofauti kati ya ´Arshi na Kursiy ni kama tofauti kati ya jangwa na pete hiyo.”[5]

Hilo pia linasambaratisha kufasiri Kursiy kwamba ni ujuzi, tafsiri ambayo haikusihi kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa), kama nilivyobainisha katika ”as-Swahiyhah” (109).

[1] 85:14-16

[2] 69:17

[3] 2:255

[4] al-Haakim amesema:

”Swahiyh kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim.” (al-Mustadrak (2/282))

adh-Dhahabiy amesema:

”Wasimulizi wake ni wenye kuaminika.” (al-´Uluww, uk. 61)

al-Azhariy amesema:

”Wanazuoni wameafikiana juu ya usahihi wa upokezi huu.” (Tahdhib-ul-Lughah (10/61))

[5] Jaamiy´-ul-Bayaan (5/399) na Abush-Shaykh katika ”al-´Adhwamah” (2/587).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 50-51
  • Imechapishwa: 29/09/2024