33. Bid´ah wakati wa kutembelea al-Madiynah al-Munawwarah

Ni katika Sunnah kufunga safari kwa ajili ya kwenda kutembelea msikiti wa kinabii na msikiti wa al-Aqswaa – tunamuomba Allaah awarudishie waislamu karibuni – kutokana na zile fadhilah na thawabu zinazopatikana kwa kufanya hivo. Hapo kabla watu walikuwa na mazowea ya kuitembelea kabla ya hajj au baada ya hajj. Wakati walipokuwa wanafanya hivo walikuwepo watu wengi ambao walikuwa wakitumbukia katika mambo yaliyozuliwa na Bid´ah, mambo yatambulikanayo kwa wanachuoni. Nimeonelea katika kukamilisha faida basi nitaje baadhi yake kwa lengo la kufikisha na kutahadharisha.

132- Kusafiri kwa ajili ya kulikusudia kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[1].

133- Mtu kuwaomba mahujaji na watembezi kumfikishia salamu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

134- Kuoga kabla ya kuingia al-Madiynah al-Munawwarah.

135- Kusema pindi mtu anapoiona al-Madiynah:

اللهم هذا حرم رسولك فاجعله لي وقاية من النار وأمانا من العذاب وسوء الحساب

“Ee Allaah! Hapa ni patakatifu pa Mtume wako. Pafanye kuwa ni ulinzi kwangu kutokamana na Moto, amani kutokamana na adhabu na hesabu mbaya.”

136- Kusema wakati wa kuingia al-Madiynah:

بسم الله وعلى ملة رسول الله

“Kwa jina la Allaah na kwa dini ya Mtume wa Allaah.”

وَقُل رَّبِّ أَدْخِلْنِي مُدْخَلَ صِدْقٍ وَأَخْرِجْنِي مُخْرَجَ صِدْقٍ وَاجْعَل لِّي مِن لَّدُنكَ سُلْطَانًا نَّصِيرًا

“Sema: “Ee Rabb wangu! Niingize mwingizo mwema na nitoe kutoka kwema na unipe nguvu zinazotoka Kwako zinazosaidia.”[2]

137- Kuwepo kwa kaburi la Mtume ndani ya msikiti.

138- Kulitembelea kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kabla ya kuswali kwenye msikiti wake.

139- Kuna ambao wanalielekea kaburi kwa unyenyekevu wa hali ya juu na huku wameweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto kama wanavofanya wakati wa kuswali. Haya yanafanywa ni mamoja mtu yuko karibu nalo au mbali, wakati wa kuingia msikitini au kutoka.

140- Kukusudia kulielekea kaburi wakati wa kuomba du´aa.

141- Kulikusudia kaburi kwa kuomba karibu nalo kwa kutarajia kujibiwa.

142- Kutawassul naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Allaah wakati wa kuomba du´aa.

143- Kuomba uombezi na mengineyo kutoka kwake.

144- Ibn-ul-Haajj amesema katika “al-Madkhal” (01/259):

“Katika adabu ni mtu asitaje mahitajio yake wala kuomba kutaka kusamehewa madhambi yake wakati wa kulitembelea kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anajua zaidi ni mahitajio gani alonayo na nini kilicho na manufaa zaidi kwake.”

145- Amesema vilevile (01/264):

“Kuhusiana yeye kuona yale Ummah wake wanafanya na kuzijua hali zao, nia zao, tawbah zao na fikira zao, basi hakuna tofauti baina ya kufa kwake na kuwa kwake hai.”

146- Mtu kuweka mkono wake kwenye dirisha la chumba lililojengwa juu ya kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ajili ya kutafuta baraka. Baadhi yao wameliapia hilo na kusema:

وحق الذي وضعت يدك شباكه وقلت: الشفاعة يا رسول الله

“Naapa kwa haki ya yule ambaye ameuweka mkono wake juu ya dirisha lake na akasema: “Uombezi, ee Mtume wa Allaah!”

147- Kubusu kaburi au kuligusa au yale yaliyo karibu na kaburi[3].

148- Kulazimiana na sura maalum wakati wa kumtembelea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na marafiki zake, kuwasalimia na kuwaombea du´aa kwa njia maalum. Kwa mfano al-Ghazaaliy amesema:

“Asimame karibu na uso wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), aelekee Qiblah na azielekee kuta za kaburi… na aseme: “Amani ya Allaah iwe juu yako, ee Mtume wa Allaah… “

Halafu akataja salamu ndefu kisha swalah na du´aa ndefu. Urefu wake ni karibu kurasa tatu[4].

149- Kukusudia kuswali kwa kulielekea kaburi.

150- Kukaa karibu na kaburi na pembezoni mwake kwa ajili ya kusoma na kufanya Adhkaar.

151- Kwenda kwenye kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ajili ya kumsalimia baada ya kila swalah[5].

152- Watu wa al-Madiynah kukusudia kulitembelea kaburi la kinabii kila pale wanapoingia msikitini au wanapotoka.

153- Kunyanyua sauti baada ya kila swalah kwa kusema:

السلام عليك يا رسول الله

“Amani ya Allaah iwe juu yako, ee Mtume wa Allaah.”

154- Kutafuta baraka kutoka kwenye vigamba vya rangi ya kijani vinavyoputukika kutoka katika kuba juu ya kaburi la kinabii.

155- Kujikurubisha kwao kwa Allaah kwa kula tende za Sayhaan kwenye Rawdhwah tukufu baina ya mimbari na kaburi.

156- Kukata sehemu ya nywele zao na kuzitupa kwenye taa kubwa lilioko karibu na kaburi la kinabii.

157- Baadhi yao wanapangusa mikono yao kwenye mitende miwili iliowekwa magharibi mwa mimbari[6].

158- Wengi wa watu kuswali sehemu kale ya msikiti na kupuuzilia mbali safu za mbele zilizozidishwa na ´Umar na wengineo.

159- Wale wanaotembelea al-Madiynah kulazimiana na kubaki hapo kwa muda wa wiki nzima mpaka waweze kuswali katika msikiti wa kinabii swalah arubaini ili waweze kuandikiwa kutakasika kwao kutokamana na unafiki na Moto[7].

160- Kukusudia kwenda katika misikiti mingine na makaburi mengine yaliyoko al-Madiynah na pembezoni mwake baada ya kutembelea msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika hiyo kunavuliwa tu msikiti wa Qubaa´.

161- Baadhi ya watu kuitwa “watembezi”. Wanawahamasisha mahujaji baadhi ya Adhkaar na nyuradi ndefu kwenye kaburi au mbali na kaburi kwa sauti za juu. Matokeo yake wale wahamasishwaji wanazirudi kwa sauti iliyo juu zaidi.

162- Kutembelea Baqiy´ kila siku na kuswali kwenye msikiti wa Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anhaa).

163- Kufanya alkhamisi ni siku maalum kwa ajili ya kuwatembelea mashahidi wa Uhud.

164- Kufunga vitambara kwenye madirisha ya makaburi ya mashahidi.

165- Kutafuta baraka kwa kuoga kwenye birika ambalo liko karibu na makaburi yao.

166- Kutoka kwenye msikiti wa kinabii kinyumenyume wakati mtu anapoaga na kurudi zake nyumbani.

[1] Sunnah ni kukuusidia msikiti. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kusifungwe safari isipokuwa kuelekea katika misikiti mitatu… “

Mtu anapofika pale na akaswali Tahiyyat-ul-Masjid ndipo anatembelea kaburi lake  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ni wajibu kwa mtu kutambua kwamba kufunga safari kwa ajili ya kutembelea kaburi lake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makaburi mengineyo na kulitembelea pasi na kufunga safari haya ni mambo mawili tofauti. Hata hivyo haya hayafanywi na hawa waliokuja nyuma. Katika wao wako mpaka madokta. Kwa sababu ya kuchanganya kwao mambo wamekosea kwa mara nyingine na kudai kwamba Salafiyyuun, na khaswakhaswa Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah), wanapinga kitendo cha kulitembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba limewekwa katika Shari´ah. Huu ni uongo wa wazi. Ukitaka rejea katika Radd yetu kwa Dr. al-Buutwiy iliochapishwa katika msururu wa makala katika gazeti la “at-Tamaddun al-Islaamiy”. Kisha nikatoa kitabu maalum nilichopita kichwa cha khabari ”Difaa´ ´an al-Hadiyth an-Nabawiy”.

[2] 17:80

[3] al-Ghazaaliy (Rahimahu Allaah) amefanya jambo zuri wakati alipokemea kubusu kulikotajwa na akasema:

“Hii ni desturi ya manaswara na mayahudi.”

Je, wako wenye kuzingatia?

[4] Kilichowekwa katika Shari´ah ni kusema:

السلام عليك يا رسول الله ورحمة الله وبركاته السلام عليك يا أبا بكر السلام عليك يا عمر كما كان ابن عمر يفعل فإن زاد شيئا يسيرا مما يلهمه ولا يلتزمه فلا بأس عليه إن شاء الله تعالى

“Amani ya Allaah iwe juu yako, ee Mtume wa Allaah, rehema Zake na baraka Zake. Amani ya Allaah iwe juu yako, ee Abu Bakr. Amani ya Allaah iwe juu yako, ee ´Umar.”

Hivi ndivo Ibn ´Umar alivokuwa akifanya. Akiongeza kitu kidogo, hakuna neno – Allaah (Ta´ala) akitaka.

[5] Hili si kwamba ni Bid´ah peke yake, bali ni kuchupa mipaka katika dini. Vilevile isitoshe ni kwenda kinyume na maneno yake (´alayhis-Salaam):

“Msilifanye kaburi langu kuwa ni sehemu ya kupatembelea mara kwa mara. Niswalieni popote mlipo, kwani hakika swalah zenu zinanifikia.”

Kitendo hichi ni sababu ya kupotea Sunnah na fadhilah nyingi. Nazo si zengine ni Adhkaar na nyuradi baada ya salamu. Wanaziacha na wanaikimbilia Bid´ah hii. Allaah amrehemu yule aliyesema:

“Hakuna mwenye kuzua Bid´ah isipokuwa hufisha Sunnah.”

[6] Hakuna faida kabisa juu ya mitende hii miwili. Imewekwa pale kwa ajili ya mapambo na kwa ajili ya kuwafitinisha watu. Mwishowe iliondoshwa – na himdi zote zinamstahikia Allaah.

[7] Hadiyth iliopokelewa juu ya hilo ni dhaifu na haisimamishi hoja yoyote. Nimebainisha kasoro zake katika ”as-Silsilah adh-Dhwa´iyfah” (364). Haijuzu kuitendea kazi kwa sababu ni uwekaji Shari´ah. Khaswa khaswa kwa kuzingatia kwamba ni jambo linaweza kuwatia kwenye uzito mahujaji wengi huku wakidhani kwamba Hadiyth ni Swahiyh. Inaweza kutokea wakapitwa na baadhi ya swalah huko na matokeo yake wakaingia hatiani, jambo ambalo Allaah amewasalimisha nalo.

Baadhi ya waheshimiwa wamesema kuwa Hadiyth yenye kuashiriwa ina nguvu kwa kumtegemea Ibn Hibbaan ambaye alionelea mmoja katika wapokezi wayo wasiojulikana kwamba ni mwaminifu. Sifa hii ni jambo lisilozingatiwa na wanachuoni wa Jarh na Ta´diyl. Miongoni mwao ni yule muheshimiwa mwashiriwa wenyewe, kama alivyoweka wazi katika Radd yake kwa al-Ghumaariy katika gazeti la ”al-Jaami´ah as-Salafiyyah” iliochapishwa India. Kuhusiana na hili rejea katika kitabu cha Shaykh ´Abdul-´Aziyz ar-Rabiy´aan ambapo kamraddi. Amefanya vizuri, akafaidisha na akabainisha udhaifu na mgongano katika maoni yake pale anaposema kuwa ni yenye nguvu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 56-59
  • Imechapishwa: 22/07/2018