33. Anaposema jambo basi yanaondoka maono mengine yote

´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kama dini ingekuwa kwa maoni, basi chini ya soksi za ngozi kulikuwa na haki zaidi ya kupanguswa kuliko juu yake. Hakika nimemuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akifuta juu ya soksi zake za ngozi.”[1]

´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Msiwazuie wake zenu kwenda misikitini wanapokuombeni ruhusa.” Bilaal bin ´Abdullaah akasema: ”Naapa kwa Allaah tutawazuia!” ´Abdullaah akamgeukia na kumtukana matusi makali ambayo sikupata kumsikia akimtukana hivyo. Kisha akasema: ”Ninakueleza kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wewe unasema: ”Naapa kwa Allaah tutawazuia!”[2]

Imekuja kwa Ibn ´Abdil-Barr ifuatavyo:

”Msiwazuie wake zenu kwenda misikitini wanapokuombeni ruhusa.” Bilaal bin ´Abdullaah akasema: ”Naapa kwa Allaah tutawazuia!” ´Abdullaah akamgeukia na kusema: “Allaah akulaani! Allaah akulaani! Allaah akulaani! Umesikia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kutowazuia.” Akasimama kutokana na hasira.”

´Abdullaah bin Mughaffal ameeleza:

”Mmoja katika ndugu zake ´Abdullaah bin Mughaffal alirusha mawe ambapo akamkataza na kumweleza: ”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuruhusa mawe na akasema: ”Halitumiki kwa kuwinda na wala halimuumizi adui, lakini linaweza kuvunja jino au kupasua jicho.” Baada ya hapo akamuona tena mtu yule akirusha mawe, akamwambia: ”Nimekusimulia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa alikataza kurusha mawe na bado unafanya? Sitaongea nawe kamwe.”[3]

Abu Qataadah Tamiym bin Nadhwiyr al-´Adawiy ameeleza:

“Tulikuwa kwa ´Imraan bin Husayn pamoja na kundi la watu na miongoni mwetu alikuwa Bashiyr bin Ka‘b. Siku hiyo ´Imraan akasema: ”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Hayaa yote ni kheri.”‘ Bashiyr bin Ka‘b akasema: ”Tunapata katika baadhi ya vitabu kuwa hayaa ni utulivu na heshima, lakini pia kuna hayaa nyingine ni udhaifu.” ´Imraan akaghadhibika mpaka macho yake yakawa mekundu na kusema: ”Je, huoni kuwa nakusimulia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wewe unapinga?” Kisha akarejea tena Hadiyth hiyo, na Bashiyr akarudia kusema hivyo. ´Imraan akakasirika zaidi mpaka tukalazimika kukariri: ”Huyu ni mwenzetu, ee Abu Najiyd. Hana shida yoyote.”[4]

Ibn Abiy Mulaykah ameeleza:

“´Urwah bin az-Zubayr alimwambia Ibn ´Abbaas: ”Umewapotosha watu.” Ibn ´Abbaas akasema: “Na kwa nini, ee ‘Urayyah?” ´Urwah akasema: “Unawaamrisha watu kufanya ‘Umrah katika siku hizi kumi na hakuna ´Umrah ndani yake.” Ibn ´Abbaas akasema: “Je, huwezi kumuuliza mama yako kuhusu hilo?” ´Urwah akasema: “Lakini Abu Bakr na ´Umar hawakufanya hivyo.” Ibn ´Abbaas akasema: “Naapa kwa Allaah hili ndilo lililokuangamizeni! Sioni vingine isipokuwa Allaah atakuadhibuni. Nakuhadithieni kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nyinyi na Abu Bakr na ´Umar.”[5]

al-Khatwiyb ameeleza: Muhammad bin Ahmad bin Rizq ametukhabarisha: ´Uthmaan bin Ahmad ad-Daqqaaq ametukhabarisha: Muhammad bin Ismaa´iyl ar-Raqqiy ametukhabarisha: ar-Rabiy´ bin Sulaymaan ametukhabarisha:

“Nilisikia ash-Shaafi‘iy baada ya bwana mmoja kumuuliza kitu, ambapo akajibu kuwa kumepokelewa kadhaa na kadhaa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Muulizaji akasema: ”Ee Abu ´Abdillaah, unasemaje kuhusu hili?” Nikamuona ash-Shaafi‘iy akianza kutetemeka na kupatwa na mshtuko. Halafu akasema: ”Nini hiki? Ni ardhi gani itanibeba na ni mbingu gani itanikinga ikiwa nitasimulia Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nisiiweke katika matendo? Ndiyo, naifanyia kazi. Ndiyo, naifanyia kazi.”

Amesema: ar-Rabiy´ ameeleza:

“Nimemsikia ash-Shaafi‘iy akisimulia Hadiyth ambapo akasema mmoja katika wale waliokuwa pale: ”Je, unaonelea hivo?” Akajibu: ”Ikiwa nitapokea Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nisiifanyie kazi, basi ninawashuhudisheni kuwa akili yangu imepotea.”[6]

[1] Abu Daawuud (162).

[2] Muslim (442), Ahmad (2/90), Abu ´Awaanah (2/57) na at-Twabaraaniy (13251).

[3] Jaamiy´ Bayaan-il-´Ilm wa Fadhwlih (2/375).

[4] Muslim (61), Ahmad (4/427, 436, 440, 442 na 445) na at-Twayaalisiy (2/41).

[5] Ahmad (1/337), Ishaaq, kama ilivyo katika “al-Matwaalib al-´Aaliyah” (1/360), al-Khatwiyb al-Baghdaadiy katika “al-Faqiyh wal-Mutafaqqih” (1/145), ambaye tamko ni lake, Ibn Hazm katika “Hajjat-ul-Wadaa´”, uk. 268-269, na Ibn ´Abdil-Barr katika “Jaamiy´ Bayaan-il-´Ilm wa Fadhwlih” (2/239-240).

[6] al-Faqiyh wal-Mutafaqqih (1/150), Manaaqib-ush-Shaafi´iy (1/474-475) ya al-Bayhaqiy na Hilyat-ul-Awliyaa’ (9/106) ya Abu Nu´aym.

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: as-Swalaah fiyn-Ni´aal, uk. 37-41
  • Imechapishwa: 23/06/2025