32. Tafsiri ya Qur-aan kutoka kichwani mwako

Kuhusu tafsiri ya Qur-aan kwa kutumia maoni binafsi ni haramu. Mu-ammal ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia: ´Abdul-A´laa ametuhadithia, kutoka kwa Sa´iyd bin Jubayr, kutoka kwa Ibn ´Abbaas, ambaye amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kusema juu ya Qur-aan pasi na elimu, basi na ajiandae makazi yake Motoni.”[1]

Wakiy´ ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia, kutoka kwa ´Abdul-A´laa ath-Tha´labiy, kutoka kwa Sa´iyd bin Jubayr, kutoka kwa Ibn ´Abbaas, ambaye amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kusema juu ya Qur-aan pasi na elimu, basi na ajiandae makazi yake Motoni.”

at-Tirmidhiy amesema: ´Abd bin Humayd ametuhadithia: Habbaan bin Hilaal amenihadithia: Suhayl bin ´Abdillaah al-Qutwa´iy ametuhadithia: Abu ´Imraan al-Juuniy ametuhadithia, kutoka kwa Jundub, ambaye amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kusema juu ya Qur-aan kwa maoni yake binafsi na akapatia bado amekosea.”[2]

at-Tirmidhiy amesema:

”Hadiyth hii ni ngeni. Baadhi ya wanazuoni wamemzungumzia Suhayl bin Abî Hazm.

“Yule mwenye kusema juu ya Qur-aan pasi na elimu, basi na ajiandae makazi yake Motoni.”

Vivyo hivyo baadhi ya wanazuoni wamesimulia kutoka kwa Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na wengineo, ya kwamba walimfanyia ukali yule ambaye anatafsiri Qur-aan pasi na elimu.

Kuhusu zile tafsiri za Qur-aan zilizosimuliwa kwa Mujaahid, Qataadah na wanazuoni wengine, isidhaniwe kuwa walitafsiri au kusema juu ya Qur-aan bila ya elimu au kwa matashi yao wenyewe. Kumepokelewa kutoka kwao yale yanayofahamisha juu ya niliyoyasema, ya kwamba hawakusema kutoka kwa nafsi zao wenyewe na bila ya elimu. al-Husayn bin Mahdiy al-Baswriy ametuhadithia: ´Abdur-Razzaaq ametuhadithia, kutoka kwa Ma´mar, kutoka kwa Qataadah, ambaye amesema:

”Hakuna ndani ya Qur-aan Aayah yoyote isipokuwa nimesikia kitu juu yake.”[3]

Amesema tena: Ibn Abiy ´Umar ametuhadithia: Sufyaan bin ´Uyaynah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, ambaye amesimulia kwamba Mujaahid amesema:

”Ningesoma kwa mujibu kisomo cha Ibn Mas’uud, basi nisingehitaji kumuuliza Ibn ´Abbaas kuhusu mengi ya Qur-aan ambayo nilimuuliza.”[4]

Kwa hivyo yeyote anayesema juu ya Qur-aan kwa maoni yake binafsi, amejikalifisha jambo asilokuwa na elimu nalo na amepita njia ambayo hakuamrishwa. Hata kama atapatia maana katika hali halisi, bado anazingatia amekosea kwa sababu hakufuata njia sahihi. Ni kama mtu anayetoa hukumu kati ya watu kwa ujinga, atakuwa Motoni hata kama hukumu yake itakuwa sahihi katika hali halisi. Hata hivyo kosa lake litakuwa na uzito mdogo kuliko yule aliyekosea – na Allaah ndiye anayejua zaidi. Vivyo hivyo Allaah (Ta´ala) amewaita waongo wale wanaotoa tuhuma za uzinzi na akasema:

لَّوْلَا جَاءُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ ۚ فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاءِ فَأُولَـٰئِكَ عِندَ اللَّـهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ

“Kwa nini hawakuleta mashahidi wanne? Midhali hawakuleta mashahidi, basi hao mbele ya Allaah ndio waongo.”[5]

Kwa hivyo mwenye kutoa tuhuma za uzinzi ni mwongo hata kama tuhuma zake ni za kweli kwa sababu ameelezea jambo ambalo haifai kwake kulielezea na amejikakama kitu asichokuwa na ujuzi nacho – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] at-Tirmidhiy (2950), aliyesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh. Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (2950).

[2] Abu Daawuud (3652) na at-Tirmidhiy (2952), ambaye amesema kuwa Hadiyth ni ngeni. Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (2952).

[3] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

[4] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

[5] 24:13

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 96-100
  • Imechapishwa: 13/04/2025