Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaharakisha kwenda pwani Badr na akatua pale tu alipofika kwenye maji. al-Hubaab bin al-Mundhiriy bin ´Amr akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hapa ulipotua Allaah ndiye kakuamrisha au ni sehemu umetua tu kwa ajili tu vita na njama.” Akajibu: “Ni sehemu nimetua kwa ajili ya vita na njama.” Ndipo akasema: “Hapa si pahali pa kutua. Tufuate ili tufike yanakoanzia maji yao. Tutaficha kisima nyuma yetu, kisha tukijengee hodhi itayokizunguka ili tuweze kunywa sisi na wao wasiweze kunywa.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapendekeza fikira yake. Allaah akawazuia Quraysh kutokamana na maji kwa mvua kali iliyonyesha. Ikawa ni adhabu kwa makafiri na neema kwa waislamu ambapo akawasahilishia ardhi na kuwakaminishia nayo. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akajengewa kakibanda ambapo atakuwa ndani yake[1].

Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatembea kwenda sehemu ya mapambano. Akawa anawaonyesha ni wapi wale viongozi wa makafiri watapouawa, mmoja baada ya mwingine:

“Hapa ndipo atapouawa fulani Allaah akitaka. Hapa ndipo atauawa fulani. Hapa ndipo atauawa fulani.”

´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Ninaapa kwa Yule ambaye kamtuma kwa haki hakuna yeyote aliyeuawa mahali kwengine isipokuwa pale alipoashiria Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

[1] Dalaa-il-un-Nubuwwah (3/35) ya al-Bayhaqiy.

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 48-49
  • Imechapishwa: 08/08/2018