Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mbora wa Ummah huu baada ya Mtume wake ni Abu Bakr as-Swiddiyq, kisha ´Umar bin al-Khattwaab halafu ´Uthmaan bin ´Affaan. Tunawatanguliza hawa watatu kama walivyotangulizwa na Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hawakutofautiana juu ya hilo.

Baada ya hawa watatu ni wale wa mashauriano watano: ´Aliy bin Abiy Twaalib, az-Zubayr, ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf, Sa´d na Twalhah. Wote walikuwa wanastahiki ukhaliyfah na wote walikuwa viongozi. Dalili yetu juu ya hilo ni maneno ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Tulikuwa, ilihali Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bado yuhai,  tukizingatia ya kwamba Abu Bakr ndiye bora na halafu ´Umar, kisha ´Uthmaan. Kisha tunanyamaza.”

Baada ya watu wa mashauriano wanakuja Muhaajiruun walioshiriki katika vita vya Badr, kisha Answaar walioshiriki katika vita vya Badr; kila mmoja kwa mujibu wa kuhajiri na kutangulia kwake katika Uislamu.”

MAELEZO

Ni wajibu kwa waislamu kuwafadhilisha Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) namna hii.

Ni jambo linalotambulika kwamba watu wa mashauriano ni wasita. Hawa watano na Sa´iyd bin Zayd. Sa´iyd bin Zayd alikuwa ni mmoja katika wale watu wa mashauriano japokuwa hakutajwa hapa. Sijui kama jina lake lilifutika katika baadhi ya nuskha au ilikuwa hivo katika asili.

Baada ya hawa watu wa mashaurino kunafuata wale waliokula kiapo ´Aqabah. Kisha kunafuata Muhaajiruun na Answaar walioshiriki katika vita vya Badr, halafu kunafuata wale waliokula kiapo chini ya mti, kisha kunafuata wale walioingia katika Uislamu kabla ya kukombolewa mji wa Makkah, wakahajiri na wakapigana vita, wale walioingia katika Uislamu baada ya kukombolewa mji wa Makkah, wakahajiri na wakapigana vita na hatimaye wale Maswahabah wadogo. Hivi ndivo wanavyotakiwa kupangwa kutokana na fadhilah.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 133-134
  • Imechapishwa: 25/04/2019