Tambua ya kwamba kila maandiko yenye kutaja kuwa baadhi ya matendo mema yanakifuta madhambi – kama vile wudhuu´, swawm ya Ramadhaan, swawm ya siku ya ‘Arafah na ya ´Aashuuraa’ na kadhalika – basi maana yake ni kufuta madhambi madogo, kwani hata ´ibaadah kubwa kama swalah tano, ijumaa hadi ijumaa nyingine na Ramadhaan hazifuti madhambi makubwa kwa mujibu wa Sunnah – basi vipi matendo mengine yasiyofikia daraja hizo?

Kwa hiyo wanazuoni walio wengi wanaona kuwa madhambi makubwa kama ribaa, uzinzi, uchawi n.k. hayafutwi na matendo mema peke yake – bali yanahitaji tawbah ya kweli au kutekelezwa kwa adhabu ya Kishari´ah pale panapohitajika adhabu hiyo.

Kwa hiyo ni wajibu kwa muislamu katika masiku haya yenye fadhilah afanye haraka kutubu kutokana na madhambi yote, madogo na makubwa, huenda Allaah (´Azza wa Jall) akamkubalia tawbah yake, akamsamehe madhambi yake na akakubali ´ibaadah zake. Kwani tawbah katika nyakati bora ina nafasi kubwa, kwa kuwa roho huwa zinakuwa tayari kwa ajili ya ´ibaadah na hupata tawbah ya kweli kwa sababu ya kutambua kosa, kujuta juu ya yaliyopita khaswa tukiwa kwenye mwanzo wa mwaka mpya. Hata hivyo tawbah ni wajibu katika nyakati zote.

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 59
  • Imechapishwa: 18/05/2025