31. Wasia wa dhahabu kutoka kwa mama kwenda kwa bintie biharusi

Naonelea ninukuu wasia wa mama aliyempa msichana wake, kwani ni wasia wenye kutosheleza kwa ambaye atauelewa vyema. Mwanamke mmoja mwenye hekima na busara, Umaamah bint al-Haarith, alimuusia binti yake wakati alipoenda kindoa kwa mume wake:

Ee msichana wangu kipenzi! Iwapo wasia unaachwa kwa sababu ya tabia njema na nasaba nzuri, basi ningeuacha kwako. Hata hivyo wasia ni ukumbusho kwa ambaye ameghafilika na ni msaada kwa mwenye busara.

Ee msichana wangu kipenzi! Endapo mwanamke angelikuwa anatosheka kuwa na mume kwa sababu ya wazazi wake wana uwezo wa kutosha na kwa sababu wazazi wake wanamuhitajia, basi wewe ungelikuwa ni mwenye kutosheka zaidi kutokana na hilo. Hata hivyo wanawake wameumbiwa waume na wanaume wameumbiwa wake.

Ee msichana wangu kipenzi! Hakika wewe umetoka katika lile pango ulilokuwa ukiishi na waacha kiota ambacho ulikuwa umezowea kukaa ndani yake na waenda maeneo usiyoyajua na kwa mwenziwe ambaye hamtambuani, basi yeye amekuwa ni mwenye kukumiliki. Kwa hivyo kuwa mbele yake kama kijakazi na hivyo yeye atakuwa mbele yako kama mtumwa. Chunga kwake yeye mambo kumi na iwe ni akiba yako:

1 & 2 – Jipambe na tabia ya kukinai na matangamano mazuri kwa kumsikiliza na kumtii. Kwani hakika ukinaifu ndio raha ya moyo na katika kutangamana naye kwa uzuri kunamridhisha Mola.

3 & 4: Yachunge vyema macho yake na chunga pale inapoangukia harufu yake. Kwa maana ya kwamba macho yake yasione kutoka kwako jambo baya na asinuse kutoka kwako isipokuwa harufu nzuri kabisa.

5 & 6: Chunga wakati wa kula kwake na pia chunga wakati wa kulala kwake, kwani joto la njaa linasababisha hasira na kukosa kulala husababisha ghadhabu.

7 & 8: Ichunge mali yake na familia yake. Msingi wa hilo ni ule upimaji wako mzuri wa namna ya utumiaji na uzuri wa namna unavyowaendesha.

9 & 10: Usimuenezee siri zake na wala usimuasi amri yake yoyote. Ukitoa siri yake, basi usijiaminishe yeye kutokufanyia khiyana. Ukiasi amri yake, basi utamtia dhiki moyoni mwake. Pamoja na hayo yote jihadhari kumuonyesha furaha wakati yeye ana huzuni na pia kuonyesha dhiki wakati yeye ana furaha. Kwani hiyo hali ya kwanza ni katika mapungufu na hiyo hali ya pili ni katika kumuharibia mudi yake. Kwa kiasi cha unavyomtukuza mume wako ndio kiasi cha vile yeye atakukirimu. Na kiasi cha utavyoafikiana naye ndio kutazidi kuendelea kuishi naye.

Tambua, ee msichana wangu kipenzi, ya kwamba hayo yote hutoweza kuyafikia mpaka utapotanguliza mbele radhi zake kabla ya radhi zako wewe, na utangulize mbele matamanio yake yeye kabla ya matamanio yako wewe kabla ya yale unayoyapenda na kuyachukia. Nakuombea kwa Allaah akujaalie kheri na nakuaga[1].

[1] Majmuu´-ul-Amthlaal (02/262-263).

  • Mhusika: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Twalaaq – asbaabuhu wa ´ilaajuh, uk. 48-50
  • Imechapishwa: 29/04/2024