31. Tafsiri ya Qur-aan kwa mujibu wa wanafunzi wa Maswahabah

Ikiwa hupati tafsiri ndani ya Qur-aan, ndani ya Sunnah wala masimulizi ya Maswahabah, maimamu wengi wamerejea katika masimulizi ya wanafunzi wa Maswahabah. Mmoja wao alikuwa ni Mujaahid bin Jabr, ambaye alikuwa alama katika kufasiri Qur-aan. Muhammad bin Ishaaq amesema: Abaan bin Swaalih ametuhadithia, kutoka kwa Mujaahid, ambaye amesema:

”Nilisoma Qur-aan yote mbele ya Ibn ´Abbaas mara tatu kuanzia mwanzo hadi mwisho wake, nikisimama kwenye kila Aayah na nikumuuliza juu yake.”

at-Tirmidhiy amesema: al-Husayn bin Mahdiy al-Baswriy ametuhadithia: ´Abdur-Razzaaq ametuhadithia, kutoka kwa Ma´mar, kutoka kwa Qataadah, ambaye amesema:

”Hakuna ndani ya Qur-aan Aayah yoyote isipokuwa nimesikia kitu juu yake.”[1]

Amesema tena: Ibn Abiy ´Umar ametuhadithia: Sufyaan bin ´Uyaynah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, ambaye amesimulia kwamba Mujaahid amesema:

”Ningesoma kwa mujibu kisomo cha Ibn Mas’uud, basi nisingehitaji kumuuliza Ibn ´Abbaas kuhusu mengi ya Qur-aan ambayo nilimuuliza.”[2]

Ibn Jariyr amesema: Abu Kurayb ametuhadithia: Twalq bin Ghannaam ametuhadithia, kutoka kwa ´Uthmaan al-Makkiy, kutoka kwa Ibn Abiy Mulaykah, ambaye amesema:

” Nilimuona Mujaahid, akiwa na mbao, akimuuliza Ibn ´Abbaas kuhusu tafsiri ya Qur-aan. Ibn ´Abbaas akimwambia: “Andika.” Mpaka akamuuliza juu ya tafsiri nzima.”[3]

Kwa ajili hiyo ath-Thawriy amesema:

”Ukifikiwa na tafsiri kutoka kwa Mujaahid, basi tosheka nayo.”[4]

Wengine ni kama Sa´iyd bin Jubayr, ´Ikrimah, mtumwa wa Ibn ´Abbaas, ´Atwaa’ bin Abiy Rabaah, al-Hasan al-Baswriy, Masruuq bin al-Ajda´, Sa´iyd bin al-Musayyab, Abul-´Aaliyah, ar-Rabiy´ bin Anas, Qataadah, adh-Dhwahhaak bin Muzaahim na wengine miongoni wanafunzi wa Maswahabah, waliowafuata na waliokuja baada yao. Wanaweza kujieleza kwa kutumia matamshi tofauti, kwa namna ya kwamba wale wasio na elimu wakafikiri kuwa ni tofauti katika maoni na hivyo kuzinukuu kama maoni tofauti, hali ambayo ukweli wa mambo sivyo. Wakati mwingine baadhi yao hueleza jambo kwa kutumia athari zake au kitu kinachofanana nacho, na wengine wakataja jambo moja kwa moja kama lilivyo. Mara nyingi maana huwa moja hata kama matamshi yanatofautiana. Hii ni jambo ambalo mwenye akili anapaswa kulitambua!

Shu´bah bin al-Hajjaaj na wengine wamesema:

“Maoni ya wanafunzi wa Maswahabah hayajengi hoja, ni vipi basi yataenga hoja katika tafsiri?”

Hii ina maana kuwa hajajengi hoja dhidi ya wale wengine waliopingana nayo. Hili ni sahihi. Hata hivyo ikiwa wataafikiana katika jambo fulani, basi hapana shaka yoyote ya kwamba ni hoja. Lakini wanapopingana, maoni ya mmoja wao hayawi hoja juu ya mwingine wala kwa wale waliokuja baada yao. Katika hali hiyo itabidi kurejea katika lugha ya Qur-aan, Sunnah, lugha ya kiarabu au maneno na masimulizi ya Maswahabah.

[1] at-Tirmidhiy (2952).

[2] at-Tirmidhiy (2952).

[3] Jaamiy´-ul-Bayaan (1/65).

[4] Jaamiy´-ul-Bayaan (1/65).

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 94-96
  • Imechapishwa: 13/04/2025