31. Kuchelewesha daku na kuharakisha kufungua

Miongoni mwa adabu za swawm ni kuchelewesha kula daku iwapo hakuogopa kuchomoza kwa alfajiri ya pili. Hilo ni kutokana na maneno ya Zayd bin Thaabit (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

”Tulikula daku pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha tukasimama kwenda kuswali.” Nikasema: ”Kulikuwa na muda gani baina ya daku na swalah?” Akasema: ”Kiasi cha aya khamsini.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth ya Abu Dharr inasema:

”Ummah wangu utaendelea kuwa katika kheri maadamu wanachelewesha daku na wanaharakisha kufungua.”[2]

Vilevile ni kwa sababu jambo hilo linatia nguvu zaidi katika kufunga. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe wa alfajiri kutokana na uzi mweusi.”[3]

Maana yake ni giza la usiku na weupe wa mchana.

Baadhi ya watu leo hukesha sehemu kubwa ya usiku, kisha wanapotaka kulala hula daku na hulala na huacha swalah ya Fajr. Hawa wamefunga kabla ya wakati wa swawm na wameacha swalah ya Fajr na wala hawajali amri za Allaah. Hisia gani walizonazo hawa juu ya dini yao, funga yao na swalah zao ilihali hawajali chochote mradi tu wanazipa nafsi zao wanachokitamani!

[1] al-Bukhaariy (1921) na Muslim (1097).

[2] Ahmad (05/172) na at-Twahaawiy (01/140).

[3] 02:187

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 33
  • Imechapishwa: 27/02/2026