Swawm ni miongoni mwa matendo bora kabisa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Miongoni mwa faida za swawm ya Sunnah – mbali na thawabu zake – ni kwamba kama ilivyo kwa ´ibaadah za Sunnah nyingine, hufidia mapungufu yaliyomo katika utekelezaji wa faradhi. Miongoni mwa hayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu swalah:

“Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema: ”Angalieni kama mja wangu ana swalah za Sunnah? Zitatumika kujazia mapungufu yaliyomo katika swalah za faradhi na matendo mengine yatakuwa hivyo hivyo.”[1]

Kadhalika swawm za kujitolea humsogeza mja karibu zaidi na Allaah (´Azza wa Jall) na kumpatia mapenzi Yake, kama ilivyo katika Hadiyth Qudsiy:

”Mja Wangu hatojikurubisha kwa chochote ninachokipenda zaidi kuliko yale niliyomfaradhishia. Mja wangu hatoacha kujikurubisha Kwangu kwa mambo ya kujitolea mpaka Nimpende.”[2]

[1] Ameipokea at-Tirmidhiy kwa ukamilifu wake kupitia kwa Abu Hurayrah  (Radhiya Allaahu  ´anh) kutoka kw Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). at-Tirmidhiy amesema:

”Hadiyth ni nzuri.”

Hata hivyo ndani yake kuna Hurayth bin Qubayswah au Qubayswah bin Hurayth, ambaye ni mnyonge. Pengine at-Tirmidhiy ameifanya kuwa nzuri kwa mkusanyiko wa njia zake.

[2] al-Bukhaariy (6502).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 58
  • Imechapishwa: 18/05/2025