31. Je, inajuzu jamii za Kiislamu zilizopo hii leo kuziita kuwa ni “za wakati wa kishirikina”?

Swali 31: Je, inajuzu jamii za Kiislamu zilizopo hii leo kuziita kuwa ni “za wakati wa kishirikina”?

Jibu: Wakati wa kishirikina ulioenea umeondoka kwa kutumwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hiyo haijuzu kuzipachika jamii za Kiislamu kwa njia yenye kuenea[1]. Hata hivyo inajuzu kuwapachika sifa hiyo baadhi ya watu, makundi au jamii. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kumwambia mmoja katika Maswahabah zake:

“Hakika wewe ni mtu mwenye chembechembe za wakati wa kishirikina.”[2]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mambo manne katika ummah wangu ni miongoni mwa mambo ya kipindi cha kikafiri na hawatoyaacha; kujifakhari kwa ukoo, kutukaniana nasaba, kuinasibisha mvua kwa nyota na kuomboleza.” [3]

[1] Huku ni kukufurisha ummah wa Kiislamu. Sayyid Qutwub alitamka hivyo maeneo mengi katika vitabu vyake. Kwa mfano Sayyid Qutwub anasema:

“Katika wigo ya wakati wa kikafiri kunaingia vilevile zile jamii za Kiislamu ambazo zinajidai kuwa ni kiislamu. Jamii hizi haziingii katika wigo huu kwa sababu wanaonelea kuwa kuna mwengine asiyekuwa Allaah anayestahiki kuabudiwa na wala sio kwa sababu wanamuabudu mwengine asiyekuwa Allaah – ni kwa sababu hawajisalimishi kwa Allaah hali ya kuwa peke yake hana mshirika katika mambo ya maisha yao. Hata kama hawaamini kuwa kuna mwingine asiyekuwa Allaah ambaye ana haki ya kuabudiwa wanampa sifa za kiungu ambazo ni maalum mwengine asiyekuwa Allaah pale wanapohukumu kwa Shari´ah isiyokuwa ya Allaah…

Hili likiwa wazi kunathibiti msimamo wa Kiislamu juu ya jamii hizi za wakati wa kishirikina kwa njia ya kukataa kuutambua Uislamu na kujisalimisha kwao.” (Ma´aalim fiyt-Twariyq, uk. 101)

Amesema tena:

“Tukitazama dunia nzima hii leo kutokana na ufahamu wa Uislamu sahihi basi hatupati kuona kuwa dini hii ina uwepo… Uwepo huu ulikatika tangu wakati ambao kikosi kubwa cha waislamu kilipoacha kuhukumu maisha ya watu na hukumu ya Allaah (Subhaanah) hali ya kuwa hana mshirika.” (al-´Adaalah al-Ijtimaa´iyyah, uk. 250)

Sayyid Qutwub amesema tena:

“Ulimwengu umekuwa kama ilivyokuwa kipindi ambapo shahaadah “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ilipokuja kwa watu. Wanaadamu wameritadi na kuanza kuwaabudia waja na wakandamizaji wa dini. Umeacha shahaadah “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” hata kama bado kuna kundi la watu lenye kukariri “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” juu ya minara bila ya kuelewa maana yake. Walimwengu kwa jumla, ikiwa ni pamoja na wale ulimwenguni mzima wanakariri katika minara neno “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” bila ya uelewa na utambuzi… watu hawa ni watenda madhambi wakubwa na wenye kustahiki adhabu kali siku ya Qiyaamah. Kwa sababu wameritadi kwa kuwaabudia waja baada ya kufikiwa na uongofu na baada ya kuwa katika dini ya Allaah.” (Fiy Dhwilaal-il-Qur-aan (02/1057))

Muhammad Suruur aliyachukua maneno haya ili kuwatukana wanazuoni na kuwatuhumu kuwa ni waja wa waja ambao ni waja wa waja ambao ni waja wa waja ambao ni waja wa waja. Mmoja katika ambao wanashuhudia Takfiyr ya Sayyid Qutwub juu ya jamii za Kiislamu ni mwenzao Yuusuf al-Qaradhwaawiy ambaye amesema:

“Katika hatua hii kukajitokeza vitabu vya Sayyid Qutwub ambaye amewakilisha fikira ya hatua yake ya mwisho. Hapa ameikufurisha jamii, kuchelewesha ulinganizi katika nidhamu ya Kiislamu… na kuita katika jihaad ya mashambulizi dhidi ya watu wote… Ni jambo lenye kujidhiri waziwazi kwenye vitabu vya shahidi ”Fiy Dhwilaal-il-Qur-aan”, ”Ma´aalim fiyt-Twariyq”, ”al-Islaam wa Mushkilaat-ul-Hadwaarah” na vinginevyo. (Awlawiyyaat-ul-Harakah al-Islaamiyyah, uk. 110)

Vivyo hivyo alishuhudia hilo Fariyd ´Abdul-Khaaliq, mmoja katika viongozi wa al-IKhwaan al-Muslimuun, pale aliposema:

”Fikira za kukufurisha zilijitokeza kati ya vijana wa al-Ikhwaan walipokuwa wametiwa jela. Yalitokea mwishoni mwa miaka ya 50 au mwanzoni mwa miaka ya 60. Waliathirika na fikira za Sayyid Qutwub na vitabu vyake. Kutokea humo wamechukua ikiwa ni pamoja na kuwa jamii ziko katika kipindi cha kishirikina na kuwakafirisha watawala wake wenye kupinga hukumu ya Allaah kwa kuhukumu kinyume na aliyoteremsha Allaah na kuwakufurisha raia wake kwa sababu wameridhia kuhukumiwa kwayo.” (al-Ikhwaan al-Muslimuun fiy Miyzaan-il-Haqq, uk. 115)

[2] al-Bukhaariy na wengine wamepokea kupitia kwa Waaswil bin al-Ahdab, kutoka kwa al-Ma´ruuf ambaye amesema:

“Nilikutana na Abu Dharr ar-Rabadhah. Yeye na mtumwa wake kila mmoja alikuwa amevaa koti lakeNikamuuliza sababu ya kufanya hivo ambapo akajibu kwa kusema: “Nilimtukana bwana mmoja na nikamkashifu kwa sababu ya mama yake. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanambia: “Ee Abu Dharr! Hivi kweli umemkejeli kwa sababu ya mama yake? ““Hakika wewe ni mtu mwenye chembechembe za wakati wa kishirikina.” (al-Bukhaariy (30))

[3] Ahmad (05/344) na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 86-89
  • Imechapishwa: 31/05/2023
  • mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy