30. Njia bora kabisa ya kutaja tofauti za maoni

Hii ndiyo njia bora zaidi ya kushughulikia tofauti za maoni; kunukuu maoni yote kikamilifu yanayohusiana na suala hilo na kisha kubainisha ni yepi sahihi kati ya maoni hayo. Jengine ni kwamba asambaratishe batili na aelezee faida ya tofauti hizo na matokeo yake ili kuepusha mijadala mirefu na mizozo juu ya mambo yasiyo na faida, ambayo hupelekea watu kupoteza muda na kuachana na mambo ya msingi na yenye umuhimu zaidi.

Kuhusu yule anayenukuu tofauti za maoni katika suala fulani lakini asikamilishe maoni yote ya watu, basi amefanya upungufu. Hii ni kwa sababu huenda maoni sahihi yapo katika yale aliyoyaacha. Pia amefanya upungufu yule ambaye ananukuu tofauti za maoni na asibainishe ipi ni sahihi kati ya hizo. Ikiwa atasahihisha yasiyo sahihi kwa makusudi, basi amekusudia kusema uwongo. Kama amefanya hivo kwa ujinga, amekosea. Vivyo hivyo yule anayebainisha tofauti za maoni katika masuala yasiyo na faida au anayetoa maoni mengi kimatamshi ambayo yanarudi katika mtazamo mmoja au mitazamo miwili kimsingi, basi amepoteza muda bure. Mtu kama huyo ni kama anayevaa mavazi ya uwongo.

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 92-93
  • Imechapishwa: 13/04/2025