Mja anaweza tu kuwa na nguvu za kutosha kuhudhuria swalah na kujishughulisha nayo pamoja na Mola wake (´Azza wa Jall) ikiwa atatiisha matamanio yake. Vinginevyo moyo ambao umeshindwa na matamanio, kufungwa na matakwa na shaytwaan ameukuta ndani yake sehemu ya kukaa na kujitawala humo, ni vipi basi moyo huo ataokoa na wasiwasi na mawazo? Nyoyo ni aina tatu:

1 – Moyo ulio tupu na hauna imani wala wema wowote. Huu ni moyo wa giza na shaytwaan amepumzika kabisa kupeleka wasiwasi humo kwa sababu tayari amefanya kuwa ni nyumba na makazi yake na ametawala humo apendavyo na amedhibiti kikamilifu.

2 – Moyo ambao umeangaziwa na nuru ya imani na taa ya imani imewashwa ndani yake, lakini bado kuna giza la matamanio na dhoruba za matakwa. Hapo shaytwaan anaingia kwa kwenda na kurudi na kuna sehemu za kujitokeza na tamaa za kupata. Basi vita inakuwa ya zamu na kurudi. Hali za aina hii hutofautiana kwa uchache na wingi. Miongoni mwao wapo ambao nyakati za kuushinda moyo wao na adui yao ni nyingi na wengine adui yao humshinda kwa nyakati nyingi zaidi. Na wapo walioko hivi mara hivi, mara hivi.

3 – Moyo uliojazwa na imani, umeangaziwa na nuru ya imani, pazia za matamanio zimeondoka na giza hizo zimefutwa. Basi kwa nuru yake ndani ya kifua kuna mng’ao na kwa ajili ya mng’ao huo kuna mwangaza unaowaka. Lau wasiwasi ungesogea, ungeungua kwa huo mwangaza. Huu ni kama mbingu iliyohifadhiwa kwa nyota. Shaytwaan anapojaribu kuifikia na kuipita hupigwa mawe na kuungua. Mbingu siyo yenye heshima kubwa zaidi kuliko muumini. Ulinzi wa Allaah (Ta´ala) kwake ni kamili zaidi kuliko ulinzi wa mbingu. Mbingu ni mahali pa ´ibaadah ya Malaika na makao ya wahy. Ndani yake kuna nuru za utiifu. Moyo wa muumini ni makazi ya upwekeshaji, mapenzi, maarifa na imani. Ndani yake kuna nuru zake. Basi ni mwenye kustahiki kulindwa na kuhifadhiwa dhidi ya hila ya adui ili asipate lolote kwake isipokuwa kwa kumwibia kwa ghafla.

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 52-53
  • Imechapishwa: 06/08/2025