30. Maiti hanufaiki kitu na kulia kwa walio hai

Itambulike kuwa kule kulia hakumnufaishi chochote yule maiti kabisa. Chenye kumnufaisha ni matendo yake. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Maiti hufuatwa na vitu vitatu; familia yake, mali yake na matendo yake. Viwili vinarudi na kimoja kinabaki. Familia na mali yake vinarejea na matendo yake yanabaki.”

al-Bukhaariy amepokea vilevile:

“Anapofariki mwanaadamu basi matendo yake yanakatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu yenye kunufaisha au mtoto mwenye kumuombea du´aa.”

Ndio maana maiti hanufaiki kwa kulia na kusononeka. Ibn-ul-Jawziy amesema:

“Nimeona watu wengi wanataabika hali ya kupitiliza wakati wa msiba. Ni kama kwamba hawatambui hiyo ndio sababu ya kuwepo dunia. Hivi kweli aliye na afya njema hungoja jengine zaidi ya ugonjwa? Mtumzima hungoja jengine zaidi ya kuingia katika umri mdhalilifu? Aliyepo anangoja jengine zaidi ya kukosekana?

Ni uzuri uliyoje wa mapokezi kuhusu mwanaume mmoja aliyekuja kwa Salaf mmoja ambaye alikuwa ameketi na kula. Mwanaume yule akamwambia kwamba kaka yake amefariki. Yule jamaa akasema: “Keti chini na ule. Hayo nimeshayajua.” Ndipo yule mwanaume akasema: “Umejuaje ilihali hakuna yeyote aliyekwambia?” Akajibu: “Allaah (Ta´ala) amesema:

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ

“Kila nafsi itaonja mauti.” 03:185

Chenye kukatazwa sio mahuzuniko. Ni kitu cha kimaumbile. Chenye kukatazwa ni kule kuhuzunika kwa kupindukia na kujikakama kama wale wenye kuchana nguo zao na kuvaa mavazi mabaya pindi mmoja katika ndugu anapoiaga dunia, kujipiga kwenye mashavu na kuwa na kipingamizi na Qadar. Haya na mambo mfano wa haya hayarudishi kile kilichokosekana. Bali ni mambo yanaashiria udhaifu wa mtu. Kinyume chake mtu anajikokotea tu adhabu na kukosa thawabu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 52-53
  • Imechapishwa: 14/10/2016