30. Katazo la kufunga Ramadhaan kabla ya kuandama mwezi

Tambueni kwamba miongoni mwa adabu muhimu za swawm ni muislamu kufunga katika wakati uliowekwa kwa mujibu wa Shari´ah. Kwa maana nyingine asitangulize wala asicheleweshe. Hivyo hafungi kabla ya kuthibiti kuanza kwa mwezi wala hafungi baada ya kumalizika kwake kwa kudhani kuwa ni sehemu yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mkimuona mwezi mwandamo fungeni na mkimuona fungueni.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

”Msifunge mpaka muuone mwezi mwandamo wala msifungue mpaka muuone.”[2]

Imepokelewa na Ahmad na an-Nasaa´iy.

Katika Hadiyth ya kwanza kuna amri ya kufunga pindi mwezi mpevu unapoonekana mwanzo na kufungua pindi unapoonekana mwisho. Maana yake ni kwamba eneo la funga ni baina ya miezi miwili mipevu tu.

Katika Hadiyth ya pili kuna katazo la kufunga kabla ya kuuona mwezi mwandamo na katazo la kufungua kabla ya kuonekana kwake. Pia limekuja katazo la wazi kuhusu kutanguliza mwezi kwa kufunga kwa nia kwamba ni sehemu ya Ramadhaan, kwa kuwa kufanya hivo ni kuongeza katika yale ambayo Allaah (´Azza wa Jall) ameweka katika Shari´ah. at-Tirmidhiy, an-Nasaa´iy, Ibn Maajah na Ibn Hibbaan wamepokea kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Msifunge kabla ya Ramadhaan.”[3]

Abu Daawuud amepokea kutoka kwake kwamba amesema:

”Msitangulize mwezi kwa kufunga siku moja wala siku mbili.”[4]

Kwa sababu hiyo limekuja katazo la kufunga siku ya shaka. ´Ammaar amesema:

”Atakayefunga siku inayotiwa shaka, basi amemuasi Abul-Qaasim (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[5]

Ameipokea Abu Daawuud na at-Tirmidhiy ambaye ameisahihisha na akasema:

”Hiki ndio kinachofanyiwa kazi kwa wanazuoni wengi.”[6]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Kwa sababu msingi na dhahiri ni kutokuwepo kwa mwezi mwendamo na hivyo kuufunga ni kuitanguliza Ramadhaan kwa siku moja, jambo ambalo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza jambo hilo.”

Misingi wa Shari´ah unathibitisha zaidi maoni haya kuliko maono mengine, kwani jambo linalotiwa shaka katika kuwajibika kwake halilazimiki kufanywa wala halipendekezwi. Kinyume chake inapendekezwa kuachwa kwa kushika tahadhari. Misingi ya Shari´ah haijakataza tahadhari wala haijaifanya iwe wajibu kwa msingi wa shaka pekee.”

Kutokana na hili tunajua ubatili wa madai ya wale wanaodai tuitegemee hesabu za falaki katika kufunga na kufungua kwetu, kwa sababu kwa kufanya hivyo wanatuita tufunge na kufungua kabla ya kuonekana mwezi mwandamo na hivyo kuitanguliza Ramadhaan kwa siku moja au mbili, kufunga siku ya shaka pamoja na makatazo mengine.

[1] al-Bukhaariy (1900) na Muslim (08/1080).

[2] al-Bukhaariy (1906) na Muslim (08/1080).

[3] Ameipokea at-Tirmidhiy (687) ambaye amesema:

”Hadiyth ya Ibn ´Abbaas ni nzuri na Swahiyh.”

[4] Ahmad (01/158), (nr. 226), ad-Daarimiy (1690), at-Tirmidhiy (688) na Ibn Khuzaymah (1912).

[5] Abu Daawuud (2334), at-Tirmidhiy (686), an-Nasaa´iy (2190) na Ibn Maajah (1645). Abu ´Iysaa at-Tirmidhiy amesema:

”Nzuri na Swahiyh.”

[6] Abu Daawuud (2334), at-Tirmidhiy (686), an-Nasaa’iy (2190) na Ibn Maajah (1645). at-Tirmidhiy amesema:

”Ni nzuri na Swahiyh.”

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 25/02/2026