Hii ndio miongozo ya Kiislamu kwa mwanamke kuhusiana na mume wake na haki zake. Lau wanawake wangelishikamana nazo basi nyumba zingeishi kwa furaha kamilifu. Kwa masikitiko makubwa kuna wanawake wasiozijua haki hizi. Kwa ajili hiyo talaka zimezidi kuwa nyingi, vipigo na magomvi.

Leo tunasikia jinsi baadhi ya wanawake walivyosahau upole wao, wamesahau uanawake wao, wamegeuka kuwa waasi na wenye jeuri kwa waume zao madhaifu. Wakiwapa waume zao kitu, wanawakosoa kwa ufakiri na kutokuwa na uwezo. Wakati anapokuja nyumbani anaanza kumpigia fujo na kukunja uso. Wakati anapotoka yeye ndio mwenye kumwongoza. Haridhiki naye. Ni mwenye kuonekana kwenye kila mlango na dirisha. Anaonyesha uso wake, au sehemu katika uso wake, kwa wanaume wasiokuwa Mahram zake. Wakati anapomzungumzisha mume wake anamweleza jinsi mwanaume mwingine anavyompa mke wake hiki na kile na amemfanyia hiki na kile, ni ubaya uliyoje alonao na vipi kulikuwa wanaume wenye dini wakamchumbia, lakini ndivyo hivyo…

Wakati anapokuwa nyumbani na mume wake anajiona kama mfungwa. Hajitii manukato. Hajipambi. Wakati mume wake anapomtazama anaudhika. Nywele zake zimekaa hovyo. Nguo zake zimechafuka. Amechafuka na amezungukwa na nguo hovyo hovyo, lakini pale tu anapotoka nje anajitia manukato na kujipamba. Huyu ndio mwanamke aloangamia ambaye mazuri yake anawapa wengine na mabaya anampa mume wake.

Wakati anapoenda kwa marafiki zake ni mwenye furaha na bashasha. Anazumgumza vizuri. Anavaa vizuri. Maneno yake na kikao chake hakichoshi. Pale tu anapokuja nyumba anageuka kuwa simba. Anapozungumza moto ndio unatoka kinywani mwake. Anapofanya kitu ni kashfa tupu. Mume wake hapati kheri yoyote kwake. Huyu ni mwanamke aloangamia kikweli. Vipi anataka kuwa mwenye kufaulu wakati ameenda kinyume na dini yake, kumkasirikisha Mola Wake na kumhuzunisha mume wake? Ni juu yake ajirudi. Hakika maisha ni mafupi.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 42-44
  • Imechapishwa: 24/03/2017