Swali 29: Muhammad Suruur Zayn-ul-´Aabidiyn anasema katika kitabu chake “Manhaj-ul-Anbiyaa´ fiyd-Da´wah ilaa Allaah”:

“Lau watu wa Nuuh wangelitamka shahaadah, basi ingeliwafaa kitu muda wa kuwa ni wenye kuendelea katika maasi yao.”[1]

Unasemaje juu ya maneno haya?

Jibu: Ni maneno batili[2]. Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba liwati ni uhalifu na ni moja katika madhambi makubwa, lakini hata hivyo sio kufuru. Anayetubu kwa Allaah (´Azza wa Jall) kutokana na shirki na akaacha kushirikisha lakini wakati huohuo akatumbukia katika liwati, amefanya dhambi kubwa. Pamoja na hivyo hakufuru. Lau watu wa Luutw wangemuabudu Allaah (´Azza wa Jall) peke yake na kutomshirikisha na chochote, lakini hata hivyo wakaendelea na dhambi ya liwati, wangelikuwa watenda dhambi kubwa. Ima Allaah angeliwaadhibu hapa duniani au huko Aakhirah au angeliwasamehe. Lakini hata hivyo wasingekuwa makafiri. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah, basi hakika amepotoka upotevu wa mbali.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Allaah siku ya Qiyaamah ataamrisha atolewe Motoni yule ambaye ndani ya moyo wake kulikuwa na imani sawa na mbegu ndogo ya hardali.”[4]

Kunakusudiwa wapwekeshaji ambao wametumbukai Motoni kwa sababu ya madhambi yao. Wataadhibiwa kisha baadaye watolewe Motoni kwa sababu ya Tawhiyd na ´Aqiydah yao. Mpwekeshaji endapo ataingia Motoni hatodumishwa humo milele. Kuna uwezekano vilevile Allaah akamsamehe na asiingii Motoni kabisa. Mjinga tu ndiye awezaye kuzungumza hivyo. Hiyo ndio njia bora zaidi tunavyoweza kumzingatia.

Haya ni maradhi makubwa. Walinganizi wengi leo wana maradhi haya. Wanalingania katika dini ya Allaah kwa ujinga. Matokeo yake wanawakufurisha watu bila ya sababu na wanaipuuza Tawhiyd[5]. Hebu wewe mtazame mjinga huyu! Anaipuuza ´Aqiydah na kulikuza jambo la liwati. Ni lipi baya zaidi? Je, shirki ni mbaya zaidi au liwati?

[1] Uk. 170

[2] Shaykh Muhammad Amaan al-Jaamiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Huenda vijana wengi wasifahamu maana ya maneno haya. Maana yake ni kwamba mtu ambaye ni mwenye kuendelea kutenda dhambi kubwa siku zote pasi na kutubu imani yake haitomfaa lolote hata kama ataamini. Hivyo lau kafiri mwenye kufanya dhambi kubwa, kama mfano wa uzinzi na liwati, ataitikia ulinganizi na kuanza kuamini, imani yake haitomfaa kitu muda wa kuwa ni mwenye kuendelea na dhambi hiyo. Kwa msemo mwingine dhambi inaifutilia mbali imani. Kwa msemo mwingine mtenda dhambi sio muumini.

Hii ni ´Aqiydah ya kina nani? Ni ´Aqiydah ya Khawaarij. Mlinganizi huyu ambaye yuko London na maswahibu wake wanalingania katika kitu gani? Wanalingania katika ´Aqiydah ya Khawaarij. Wanachotaka ni kuunda nchi ilio na ´Aqiydah ya Khawaarij. Khawaarij ndio wenye kusema kuwa mtenda dhambi kubwa mwenye kufa  kabla ya kutubu amekufa kama kafiri na haitomfaa kitu imani yake. Khawaarij ndio wale waliomfanyia uasi na kumkufurisha ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh).” (Kanda ambayo aliraddiwa Muhammad Suruur Zayn-ul-´Aabidiyn)

[3] 04:116

[4] al-Bukhaariy (22).

[5] Kuna mmoja wao amesema alipokuwa anafanya masomo ya Tawhiyd si lolote wala si chochote ambayo Manabii na Mitume waliwalingania watu wao kwayo kwa miaka mingi:

“Suala la Tawhiyd na kumpwekesha Allaah (Ta´ala) katika ´ibaadah ni jambo muhimu zaidi na ndio msingi. Mitume wote walilingania kwayo… Ni jambo jepesi la lililo wazi lisilosumbua. Watu wote wanalifahamu… Sehemu ya wepesi ni wepesi unaopatikana katika ´Aqiydah. Ina maana ya kwamba unaweza kumfafanulia ´Aqiydah mtu yoyote ndani ya takriban dakika kumi ili aweze kuielewa na kuifahamu kwa usahali wowote ule.” (Haakadhaa ´allam-al-Anbiyaa´, uk. 43-44)

Ikiwa mambo kweli ni hivyo, basi mtu anaweza kujiuliza ni kwa nini Sayyid Qutwub, Hasan al-Bannaa na wafuasi wao  wengine ambao walikosea katika ´Aqiydah na wakaifahamu Tawhiyd kimakosa ndani ya miaka kumi, seuze dakika kumi. Ni kwa nini baadhi yenu mnaanza mihadhara yenu kwa kuitaka msaada damu na moyo wake?

Ikiwa mambo kweli ni hivyo, basi mtu anaweza kujiuliza ni kwa nini Allaah alituma Mtume baada ya mwingine na kumfanya Nuuh (´alayhis-Salaam) akawalingania watu wake katika Tawhiyd miaka 950:

وَمَا آمَنَ مَعَهُ إِلَّا قَلِيلٌ

”Hawakuamini pamoja naye isipokuwa wachache.” (11:40)

Ikiwa mambo ni hivyo, basi mtu anaweza kujiuliza ni kwa nini Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilingania katika Tawhiyd miaka kumi na tatu Makkah. Ni kwa nini alikuwa akikariri katika kila Khutbah ya ijumaa:

“Ninakutahadharisheni na Bid´ah, kwani hakika kila chenye kuzuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”? (Muslim (867))

Ni kwa nini alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilihali yuko katika hali ya kukata roho:

“Allaah awalaani mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.”? (al-Bukhaariy (1265))

Njiani walipokuwa wanaelekea Hunayn baadhi ya Maswahabah walisema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ee Mtume wa Allaah! Hebu tuache na sisi tutundike silaha kwenye mti kama ambavyo wanafanya wao.” (Ibn Hibbaan (6702))

Ni kwa nini waarabu wale – ambao walikuwa ni mabingwa na wakiifahamu lugha ya kiarabu vizuri kuliko wengine – hawakutosheka na dakika kumi au siku kumi au ishirini ambazo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa pamoja nao baada ya kutekwa Makkah au kabla ya Hunayn?

Hivyo basi walinganizi na wengine wanatakiwa kutambua ya kwamba mafunzo ya Tawhiyd ni jambo kubwa na ni muhimu kuyakariri. Uhakika wa mambo na historia inajulisha juu ya hilo. Bali maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye hazungumzi kwa matamanio yanafahamisha hivo pale aliposema:

“Kila baada ya miaka mia Allaah hutuma mtu mwenye kuihuisha dini ya ummah huu.” (Abu Daawuud (4291). Tazama “Fath-ul-Baariy” (13/295))

Lau ingelikuwa ni jambo la sahali kuifunza Tawhiyd basi Allaah asingemlituma mtu mwenye kuihuisha yaliyopotezwa katika dini hii – na mengi ambayo watu wamepoteza ni Tawhiyd.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 82-85
  • Imechapishwa: 31/05/2023
  • mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy