29. Jeshi la Allaah ni lenye kushinda kwa ulimi na kwa silaha

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Jeshi la Allaah ndio wenye kushinda kwa hoja na kwa ulimi, kama ambavyo wanashinda kwa panga na kwa mikuki.

MAELEZO

Mtunzi (Rahimahu Allaah) anabainisha kuwa jeshi la Allaah, ambao ni waumni wenye kumnusuru Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanapambana na watu kwa njia mbili:

1 – Hoja na ubainifu. Hili ni kwa wanafiki ambao hawadhihirishi uadui dhidi ya waislamu. Watu hawa wanapambanwa kwa hoja na ubainifu.

2 – Panga na mikuki. Hili ni kwa wale wenye kudhihirisha uadui dhidi ya Uislamu. Watu hawa ni makafiri. Allaah (´Azza wa Jall) amesema juu ya watu aina hizi mbili:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ جَاهِدِ الْكُفَّارَ وَالْمُنَافِقِينَ وَاغْلُظْ عَلَيْهِمْ ۚ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ

“Ee Nabii! Pambana jihaad na makafiri na wanafiki na kuwa mshupavu kwao na makazi yao ni [Moto wa] Jahannam – napo ni mahali pabaya mno pa kuishia!” (66:09)

Wale makafiri wenye kudhihirisha ukafiri wao, wanapambanwa kwa hoja na ubainifu kwanza. Kisha baada ya hapo ndio mtu anawachukulia panga na mikuki. Wasipigwe vita kwa panga na mikuki isipokuwa baada ya kuwasimamishia hoja.

Ni wajibu juu ya Ummah wa Kiislamu kukabiliana na kila silaha yenye kuelekezwa dhidi ya Uislamu kwa njia nzuri iwezekanayo. Wale wenye kuupiga vita Uislamu kwa fikira na maneno, ni wajibu wapigwe vita kwa kufichukua upotevu wao kwa dalili za kinadharia na za kiakili. Wale wenye kuupiga vita Uislamu kwa njia ya uchumi, hawatopigwa vita peke yake, bali na wao wanatakiwa kushambuliwa kama jinsi wao wanavyoushambulia Uislamu. Hata hivyo hili linatakiwa kufanywa kama kuna uwezekano wa kufanya hivo. Kuhusu wale wenye kuushambulia Uislamu kwa silaha, ni wajibu kujihami kwa silaha mfano wake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 51
  • Imechapishwa: 04/11/2023