29. Hadiyth “Siku ya ‘Aashuuraa’ ilikuwa ikifungwa na watu wa Quraysh… ”

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Siku ya ‘Aashuuraa’ ilikuwa ikifungwa na watu wa Quraysh katika zama kabla ya kuja Uislamu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiifunga katika zama kabla ya kuja Uislamu. Alipofika Madiynah aliifunga na akaamrisha ifungwe. Lakini ilipofaradhishwa Ramadhaan akaiacha siku ya ‘Aashuuraa’. Hivyo basi anayetaka anaweza kuifunga na anayetaka anaweza kuiacha.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

MAELEZO

Hadiyth hii ni dalili kwamba watu wa zama kabla ya kuja Uislamu walikuwa wakiijua siku ya ‘Aashuuraa’ na kwamba ilikuwa ni siku maarufu kwao. Walikuwa wakiifunga na hata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pia alikuwa akiifunga. Aliendelea kuifunga kabla ya Hijrah, lakini hakuwaamrisha watu kuifunga, jambo ambalo linajulisha utukufu wa siku hii na nafasi yake ya juu kwa waarabu wa zama kabla ya kuja Uislamu hata kabla ya kutumwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu hiyo walikuwa wakifunika Ka´bah katika siku hiyo, kama ilivyo katika Hadiyth nyingine ya ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambapo amesema:

“Walikuwa wakiifunga siku ya ‘Aashuuraa’ kabla ya kufaradhishwa Ramadhaan na ilikuwa ni siku ambayo Ka´bah ilikuwa ikifunikwa…”

Ameipokea al-Bukhaariy.

al-Qurtwubiy amesema:

“Hadiyth ya ‘Aaishah inafahamisha kuwa swawm ya siku hii ilikuwa inajulikana kuwa ni yenye kusuniwa Kishari´ah na kuwa na daraja maalum. Huenda walikuwa wakitegemea katika kuifunga kuwa ni miongoni mwa Shari´ah ya Ibraahiym na Ismaa´iyl (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam), kwani walikuwa wakijihusianisha nao na kuiga hukumu zao katika mambo mengi ya Hajj na mengineyo…”

Kutokana na jumla ya dalili ni kwamba inafahamisha kuwa swawm ya ‘Aashuuraa’ ilikuwa ni lazima katika mwanzo wa kuhamia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) huko Madiynah kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi kati ya mitazamo miwili ya wanazuoni, kwa sababu amri ya kufunga ipo wazi. Salamah bin al-Akwa’ (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamuru mtu mmoja wa kabila la Aslam kutangaza kwa watu: ”Yeyote aliyekula basi afunge kilichobaki cha siku hiyo na ambaye hakula basi afunge, kwani leo ni siku ya ‘Aashuuraa’.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Baada ya kufaradhishwa Ramadhaan katika mwaka wa pili wa Hijrah, wajibu wa kufunga ‘Aashuuraa’ ukafutwa na ukabaki kuwa ni jambo la kupendelewa. Amri ya kufunga ‘Aashuuraa’ haikutokea isipokuwa mwaka mmoja tu, ambao ni mwanzo wa mwaka wa pili wa Hijrah, ambapo ‘Aashuuraa’ ilifaradhishwa mwanzoni mwa mwaka huo, kisha Ramadhaan ikafaradhishwa katikati ya mwaka huo. Katika mwaka wa mwisho wa maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – yaani mwaka wa kumi wa Hijrah – alikusudia kutofunga ‘Aashuuraa’ peke yake, bali aifunge pamoja na siku ya tisa, kama itakavyokuja huko mbele – Allaah akitaka. Na hilo ni mojawapo ya namna za kutofautiana na watu wa Kitabu katika namna yao ya kufunga.

[1] al-Bukhaariy (2007) na Muslim (1135) na kuna Hadiyth nyingine inayoitia nguvu kutoka kwa ar-Rubayy’ bint Mu’awwidh kwa al-Bukhaariy (1960) na Muslim (1136) na nyenginezo zinazoitia nguvu kwa Ahmad  na wengineo.

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 54-56
  • Imechapishwa: 18/05/2025