Jengine ni kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) amewahimiza waja Wake kuizingatia Qur-aan, kuzieleza Aayah na kufahamu maana yake katika maeneo mengi ndani ya Qur-aan Tukufu. Amesema (Subhaanah):

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا

“Je, hawaizingatii Qur-aan au nyoyoni mwao mna kufuli?”[1]

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ ۚ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِندِ غَيْرِ اللَّـهِ لَوَجَدُوا فِيهِ اخْتِلَافًا كَثِيرًا

“Je hawaizingatii Qur-aan? Na lau ingelikuwa imetoka kwa asiyekuwa Allaah, bila shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi.”[2]

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُوْلُوا الْأَلْبَابِ

“Kitabu Tumekiteremsha kwako chenye baraka ili wapate kuzingatia kwa makini Aayah zake na ili wapate kukumbuka wale wenye akili.”[3]

وَلَقَدْ ضَرَبْنَا لِلنَّاسِ فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ مِن كُلِّ مَثَلٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ قُرْآنًا عَرَبِيًّا غَيْرَ ذِي عِوَجٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ

”Hakika Tumewapigia watu mifano ya kila aina katika hii Qur-aan ili wapate kukumbuka. Qur-aan ya kiarabu isiyo na kombo ili wapate kumcha Allaah.”[4]

”Hakika Sisi tumekiteremsha kikisomeka kwa kiarabu ili mpate kufahamu.”[5]

Kuna Aayah nyingi zenye maana kama hii.

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Amehimiza kuizingatia, kuielewa, kuifahamu, iwekwe kwenye kumbukumbu na wala hakubagua chochote. Bali kuna Aayah kadhaa zinatamka wazi ueneaji, mfano wa maneno Yake:

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا

“Je, hawaizingatii Qur-aan au nyoyoni mwao mna kufuli?”[6]

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ ۚ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِندِ غَيْرِ اللَّـهِ لَوَجَدُوا فِيهِ اخْتِلَافًا كَثِيرًا

“Je hawaizingatii Qur-aan? Na lau ingelikuwa imetoka kwa asiyekuwa Allaah, bila shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi.”[7]

Ni jambo linalotambulika ya kwamba kupingwa kupingana hakukuwi isipokuwa kwa kuizingatia yote, si vinginevyo. ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alipoulizwa kama kuna maandiko mengine yoyote ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliwaachia, akasema:

“Hapana, naapa kwa Yule aliyeipasua mbegu na kuiumba nafsi! Isipokuwa ufahamu ambao Allaah humpa mja Wake wa Kitabu Chake, na kile kilichomo ndani ya ganda hili.”[8]

Akaeleza ya kwamba ufahamu ni wenye kutofautiana katika ummah. Ufahamu ni maalum zaidi kuliko elimu na hekima. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَفَهَّمْنَاهَا سُلَيْمَانَ ۚ وَكُلًّا آتَيْنَا حُكْمًا وَعِلْمًا

”Tukamfahamisha Sulaymaan kadhia hiyo; na kila mmoja Tulimpa hekima na elimu.”[9]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pengine mfikishaji akawa na ufahamu bora zaidi kuliko msikilizaji.”[10]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Fikisheni kutoka kwangu ijapo Aayah.”[11]

Isitoshe Maswahabah, waliokuja baada yao na ummah wote wamezungumzia kuhusu Aayah zote za Qur-aan, zinazohusiana na sifa na nyinginezo, wakazifasiri kwa kuzingatia dalili zake na ubainifu wake na wakasimulia Hadiyth nyingi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) zinazoafikiana na Qur-aan. Maimamu wa Maswahabah walikuwa na sehemu kubwa ya haya kuliko wengine wote. Mfano wa ‘Abdullaah bin Mas’uud, ambaye amesema:

“Kama ningelijua kuwa kuna mtu ambaye ana elimu zaidi ya Kitabu cha Allaah kuliko mimi, ningelimpanda ngamia kumwendea.”[12]

Mwingine alikuwa ni ´Abdullaah bin ´Abbaas ambaye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimwombea du´aa. Alikuwa mwanachuoni wa ummah na mfasiri wa Qur-aan. Miongoni mwa Maswahabah na wale waliokuja baada yao walikuwa miongoni mwa wanaothibitisha zaidi Sifa hizo na kuzipokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeyote ambaye ana uzoefu na Hadiyth na tafsiri ya Qur-aan anatambua jambo hilo. Hakuna katika wanafunzi wa Maswahabah ambao walikuwa watukufu zaidi kuliko maswahiba wa mabwana wawili hawa. Bali watatu wao mtukufu zaidi wanaweza vilevile kujumuishwa maswahiba wa Zayd bin Thaabit. Hata hivyo, maswahiba zake hawakusoma kwake tu, bali walisoma pia kwa ´Umar, Ibn ´Umar na Ibn ´Abbaas. Lau kama maana ya Aayah hizi zingekuwa ni zenye kukanushwa au kunyamaziwa, basi wanazuoni wa Maswahabah wa kiola, wanavyuoni wa Qur-aan na Sunnah, wasingezizungumzia zaidi kuzihusu kuliko mtu mwingine yeyote. Jengine ni kwamba Maswahabah wenyewe wamesimulia kwamba walikuwa wakijifunza kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tafsiri pamoja na kisomo. Kamwe hakuna hata mmoja wao aliyesema kwamba alikataa kufasiri Aayah yoyote. Abu ´Abdir-Rahman as-Sulamiy amesema:

“Wale waliokuwa wakitufunza Qur-aan – ´Uthman bin Affaan, ´Abdullaah bin Masuud na wengine – wametusimulia: “Ilikuwa tukihifadhi Aayah kumi na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), basi hatuzivuki mpaka tujifunze elimu na matendo yanayopatikana ndani yake.” Kwa hivyo wakatufunza Qur-aan, elimu na vitendo.”[13]

Vivyo hivyo hata maimamu walikuwa wanapoulizwa kitu kinachohusiana na hayo basi hawakanushi maana yake, bali wanathibitisha maana na kukanusha namna. Mfano wa hilo Maalik bin Anas alipoulizwa:

“Ee Abu ‘Abdillaah:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[14]

Amelingana juu vipi?” Akajibu: “Kulingana juu kunatambulika na namna haitambuliki. Ni wajibu kuamini jambo hilo na kuuliza juu yake ni Bid´ah.”

Kadhalika Rabiy’ah kabla yake. Watu wamepokea jibu hili kwa kulikubali. Hakuna yeyote katika Ahl-us-Sunnah anayelikataa.”[15]

[1] 47:24

[2] 4:82

[3] 38:29

[4] 39:27-28

[5] 12:02

[6] 47:24

[7] 4:82

[8] al-Bukhaariy (3047).

[9] 21:79

[10] Ibn Maajah (191).

[11] al-Bukhaariy (3461).

[12] al-Bukhaariy (5002) na Muslim (2463).

[13] Ahmad (5/410).

[14] 20:5

[15] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/307-309).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 48-50
  • Imechapishwa: 01/12/2025