´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si katika sisi yule mwenye kujipiga kwenye mashavu, kuchana nguo na akatamka matamshi ya kipindi cha kishirikina.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Abu Burdah ameeleza kuwa Abu Muusa alihisi maumivu kiasi cha kwamba akazimia. Kipindi hicho alikuwa ameweka kichwa chake kwenye mapaja ya mmoja katika wanawake wake. Mwanamke yule akaanza kupiga kelele, lakini hakuweza kumwambia kitu. Alipopata fahamu akasema: “Hakika mimi najitenga mbali na yale aliyojitenga kwayo mbali Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amejitenga mbali na mwanamke anayenyanyua sauti yake, kunyoa nywele zake na mwenye kuchana nguo zake wakati wa msiba.

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Umm ´Atwiyyah amesema:

“Pindi tulipokuwa tukimpa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kiapo cha usikivu na utiifu basi alikuwa akitutaka tusijiadhibu.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Abu Maalik al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Katika Ummah wangu kuna mambo mane ya kipindi cha kishirikina ambayo hayatoachwa; kujifakhari kwa kabila, kutukaniana nasabu, kuinasibisha mvua na nyota na kuomboleza.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kutoka kwa Abu Maalik al-Ash´ariy ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke mwenye kuomboleza na asitubie kabla ya kufa, basi atafufuliwa siku ya Qiyaamah akiwa amevaa mavazi ya lami na kanzu ya ukurutu.”

Katika Hadiyth ya Jaabir kuhusu Ibraahiym, mtoto wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kumetajwa ya kwamba watu walimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Hukatazi kulia?” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hapana. Nilikataza vitu viwili vya ujinga na sauti ya dhambi; sauti wakati wa msiba…. “

Ameipokea at-Tirmidhiy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 49-50
  • Imechapishwa: 14/10/2016