28. Allaah kuzungumza na waja siku ya Qiyaamah

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Inatakiwa kuamini kuwa Allaah atawazungumzisha waja siku ya Qiyaamah, hakuna baina yao na baina Yake mkalimani. Hili linatakiwa kuaminiwa na kusadikishwa.

MAELEZO

Hili ni moja katika misingi ya Ahl-us-Sunnah kuamini kwamba Allaah (´Azza wa Jall) siku ya Qiyaamah atawazungumzisha waja Wake. Ni maneno yanayolingana na ukubwa na utukufu Wake. Ni ya hakika. Waja watamsikia na kumjibu. Hadiyth inasema:

“Siku ya Qiyaamah Allaah (´Azza wa Jall) atasema: “Ee Aadam!” Ajibu: “Nimekuitikia na nakuomba furaha.” Ataitwa kwa sauti: “Allaah anakuamrisha kutoa kundi la watu kutoka katika kizazi chako kutoka ndani ya Motoni.” Aseme: “Ee Mola! Ni wangapi wametumwa Motoni?” Allaah aseme: “Mia tisa tisini na tisa ya elfumoja.”[1]

Hadiyth ni dalili inayothibitisha wito wa Allaah (Ta´ala) siku ya Qiyaamah.

“Hakuna yeyote katika nyinyi isipokuwa atazungumzishwa na Mola wake na kutakuwa hakuna baina yao mkalimani.”[2]

Atamzungumzisha mmoja mmoja. Waumini watayakubali madhambi yao.

Peponi pia atawaita na atawazungumzisha. Hii itakuwa ni neema kubwa kwa waja Peponi. Atawakirimu na kuwaneemesha. Kisha warudi katika makazi yao Peponi, hali ya kuwa wamezidi kuwa wazuri na warembo zaidi kuliko hapo kabla. Ni moja katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini jambo hilo, pasi na kulifanyia namna, ukanushaji, ufananishaji wala kulipigia mfano.

[1] al-Bukhaariy (7483) na Muslim (222).

[2] al-Bukhaariy (6539) na Muslim (1016).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 84
  • Imechapishwa: 15/10/2019