278. Ni ipi hukumu ya wanawake kuyatembelea makaburi kwa ujumla na khaswa kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Swali 278: Ni ipi hukumu ya wanawake kuyatembelea makaburi kwa ujumla na khaswa kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Jibu: Ni haramu kwa wanawake kuyatembelea makaburi. Bali ni katika madhambi makubwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanawake wanaoyatembelea makaburi na wale wanaoyafanya ni mahali pa kuswalia na wanaoyaweka mataa. Mwanamke ni dhaifu, mwenye hisia za karibu na mwenye kuathirika haraka. Kuyatembelea kwake makaburi kunapatikana madhara mengi. Pengine kitendo cha mwanamke kuyatembelea makaburi ikapelekea makaburi kujaa wanawake. Inaweza pia kupelekea watenda madhambi kuanza kuwatongoza wanawake makaburini. Kikawaida makaburi yanakuwa mbali na maeneo wanapoishi watu. Hivyo kukatokea shari kubwa. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwalaani kwake wanawake wenye kuyatembelea makaburi kunatokana na hekima kubwa.

Hata hivyo hapana vibaya endapo mwanamke atapita karibu na makaburi bila ya kukusudia kuyatembelea na akasimama na kutoa salamu iliyowekwa katika Shari´ah:

السَّلامُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الدِّيَارِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُسْلِمِين وَإِنَّا إِنْ شَاءَ اللهُ بكم لاحِقُونَ نَسْأَلُ الله لَنَا وَلَكُمْ الْعَافِية

“Amani ya Allaah iwe juu yenu manyumba ya wakazi waumini. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana nanyi. Allaah awarehemu wenye kutangulia katika sisi na nyinyi na wataokuja nyuma. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya.”

Hakika ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nini anachotakiwa kusema wakati anapopita karibu na makaburi ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akambainishia du´aa hii iliyotajwa. Lakini kukusudia kuyatembelea ni jambo la haramu na ni pia ni dhambi kubwa.

Kuhusu wanawake kulitembelea kaburi lake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), udhahiri ni kwamba ni jambo linaloingia katika ueneaji. Kwa maana nyingine mwanamke asitembelee makaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Baadhi ya wanawake wamesema kuwa inafaa kwake kulitembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu haliko wazi kama yalivyo makaburi mengine. Bali limezungushiwa kuta tatu. Kwa hiyo akilitembelea anakuwa hakulitembelea kihakika; bali amesimama nyuma yake. Lakini hapana shaka kwamba jambo hilo kidesturi linazingatiwa kuwa ni matembezi, kwa hiyo asilitembelee. Hata hivyo inatosha kwake kusema:

السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته

“Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume!”

Amswalie Mtume kwa sababu salamu yake inamfikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na analipwa thawabu kwayo.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/318-319)
  • Imechapishwa: 02/02/2026