277. Anapata hedhi kila anapotembelea kaburi

Swali 277: Mwanamke kila anapotembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapata ada yake ya mwezi. Je, hiyo ni dalili inayoonyesha kuwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamemkasirikia? Nifanye nini ili niweze kupata mapenzi ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Jibu: Haikuwekwa katika Shari´ah kwa mwanamke kulitembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amekataza kitendo hicho pale aliposema:

“Allaah amewalaani wanawake wenye kuyatembelea makaburi na wale wenye kuyafanya ni mahali pa kuswalia na kuyaweka mataa.”[1]

Kutokana na haya haitakiwi kwa mwanamke kulitembelea kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akibaki mahali pake na akamsalimia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi anafikiwa na salamu yake.

Jambo jingine ni kwamba anapata mapenzi ya Allaah kwa kumpenda na kufuata maamrisho Yake na maamrisho ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Subhaanah):

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi. Hivyo atakupendeni Allaah na atakusameheni dhambi zenu na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[2]

Kwa hiyo hakikisha unamtii Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kuwa ni mwenye kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall) na kufuata uongofu wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa njia hiyo ndio utapata maisha mazuri na malipo mema huko Aakhirah. Amesema (Ta´ala):

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Yule mwenye kutenda mema katika wanamme au wanawake – ilihali ni muumini – basi Tutamhuisha maisha mazuri na tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda.”[3]

[1] Abu Daawuud (3236), at-Tirmidhiy (320), an-Nasaa’iy (2043) na Ahmad (2030). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (225).

[2] 3:31

[3] 16:97

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/317-318)
  • Imechapishwa: 30/05/2022