Kwa hivyo ikiwa hukupata tafsiri ndani ya Qur-aan wala ndani ya Sunnah, utarejea kwenye masimulizi ya Maswahabah, kwa sababu wao walikuwa na uelewa mzuri zaidi wa Qur-aan kutokana na kushuhudia kushushwa kwake na kufahamu hali zilizohusiana nayo. Jengine ni kwamba walikuwa na akili timamu, elimu sahihi na matendo mema, khaswa wanazuoni na wakuu wao, kama vile wale maimamu wanne makhaliyfah waongofu na maimamu waongofu, kama vile ´Abdullaah bin Mas’uud. Imaam Abu Ja´far Muhammad bin Jariyr at-Twabariy amesema: Abu Kurayb ametuhadithia: Jaabir bin Nuuh ametuzindua: al-A´mash ametuzindua, kutoka kwa Abudh-Dhwuhaa, kutoka kwa Masruuq, ambaye amesimulia ya kuwa ´Abdullaah – kwa maana Ibn Mas´uud – amesema:
”Naapa kwa Yule ambaye hakuna mungu wa haki isipokuwa Yeye! Hakuna Aayah yoyote ndani ya katika Kitabu cha Allaah iliyoteremshwa isipokuwa mimi najua imeteremshwa kwa nani na wapi iliteremshwa. Kama ningelijua kuwa kuna mtu ambaye ana elimu zaidi ya Kitabu cha Allaah kuliko mimi, ningelimpanda ngamia kumwendea.”[1]
al-A’mash pia amesimulia kutoka kwa Abu Waa-il, kutoka kwa Ibn Mas’uud, ambaye ameeleza:
“Ilikuwa mmoja wetu anapojifunza Aayah kumi, basi hazivuki kabla ya kufahamu maana yake na kuzitendea kazi.”
Mtu mwingine ambaye alikuwa na elimu iliyobobea, binamu yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mfasiri wa Qur-aan. Hilo ni kutokana na baraka ya za du´aa yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alpaliposema:
“Ee Allaah! Mpe ufahamu wa dini na umfundishe tafsiri ya Qur-aan!”[2]
Ibn Jariyr amesema: Muhammad bin Bashshaar ametuhadithia: Wakiy´ ametuzindua: Sufyaan ametuzindua, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Muslim: ´Abdullaah bin Mas´uud amesema:
”Ibn ´Abbaas ni mbora wa wafasiri wa Qur-aan!”[3]
Kisha akapokea tena kutoka kwa Yahyaa bin Daawuud, kutoka kwa Ishaaq al-Azraq, kutoka kwa Sufyaan, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Muslim bin Subayh Abudh-Dhwuhaa, kutoka kwa Masruuq, kutoka kwa Ibn Mas´uud, ambaye amesema:
”Ibn ´Abbaas ni mbora wa wenye kufasiri Qur-aan!”[4]
Kisha akapokea hayohayo kutoka kwa Bundaar, kutoka kwa Ja´far bin ´Awn, kutoka kwa al-A´mash.
Kisha At-Tabari akasimulia tena kwa njia tofauti kwamba Ibn Mas’ud alisema:
“Hakika, Ibn Abbas ni mfasiri bora wa Qur’an.”
Cheni hii ya masimulizi ya Ibn Mas´uudd juu ya Ibn ´Abbaas ni sahihi. Ibn Mas’uud alifariki mwaka wa 33 kwa mujibu wa maoni sahihi. Ibn ´Abbaas aliishi miaka 36 baada yake. Fikiria ni kiasi gani cha elimu Ibn ´Abbaas alipata baada ya Ibn Mas’uud?
al-A’mash pia amesimulia kuwa Abu Waa-il amesema:
”´Aliy alimuweka ´Abdullaah bin ´Abbaas kuwa kiongozi wa msafiri wa hijjah ambapo alipowakhutubia akasoma Suurah ”al-Baqarah” – upokezi mwingine umetaja Suurah ”an-Nuur”. Akaifasiri kwa namna fulani, endapo warumi, waturuki na watu wa Daylam wangesikia, wangeingia katika Uislamu.”[5]
Kwa ajili hiyo mara nyingi Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Suddiy Mkubwa anasimulia ndani ya tafsiri yake ya Qur-aan kutoka kwa mabwana wawili hawa wakubwa: Ibn Mas´uud na Ibn ´Abbaas.
[1] al-Bukhaariy (5002) na Muslim (2462-2463).
[2] Ahmad (2879) na Ibn Hibbaan (7055).
[3] Jaamiy´-ul-Bayaan (1/65).
[4] Jaamiy´-ul-Bayaan (1/65).
[5] Jaamiy´-ul-Bayaan (1/60).
- Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 87-90
- Imechapishwa: 08/04/2025
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window) Telegram
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window) WhatsApp
- Click to print (Opens in new window) Print
- Click to email a link to a friend (Opens in new window) Email
- Click to share on Facebook (Opens in new window) Facebook
- Click to share on X (Opens in new window) X
- Click to share on Pocket (Opens in new window) Pocket