27. Sharti ya tano ya swalah ni kuondoa najisi sehemu tatu

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya tano ni kuondosha najisi yote sehemu tatu; kwenye mwili, kwenye nguo na mahali pa kuswalia. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ

 “Nguo zako zisafishe.”[1]

MAELEZO

Maana yake ni kwamba mtu kabla ya swalah yake aondoe yale yaliyoko juu ya mwili wake, nguo zake na katika sehemu anayoswalia ikiwa kuna najisi, jambo ambalo linafanyika kwa kusafisha kwa maji. Akiswali na kuna najisi na akajua baada ya kumaliza swalah, basi swalah yake ni sahihi. Akijua katikati ya swalah yake na akaweza kuvua kile chenye najisi, basi atakivua na kuendelea katika swalah yake, na kama haiwezekani, basi ataikata. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalisha Maswahabah wake na kwenye viatu vyake kulikuwa na najisi, akavivua katikati ya swalah yake na akawajulisha baada ya kumaliza ya kuwa Jibriyl alimjulisha kuwa vilikuwa na najisi.

Imepokewa na Abu Daawuud (650) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh).

Kule Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuendelea na swalah yake baada ya kuvua viatu vyake kumefahamisha juu ya usahihi wa swalah ya aliyeswali na yuko na najisi na hilo lisitambulike isipokuwa baada ya kumaliza swalah, kwani lau kama haingekuwa sahihi, basi angelazimika kuanza upya swalah kutoka mwanzo. Hili ni tofauti na anayeswali ilihali yuko na hadathi, kwani akijua katikati ya swalah ataikata, na akijua baada ya kuimaliza, atairudia swalah hiyo. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah hakubali swalah ya mmoja wenu anapokuwa na hadathi mpaka atawadhe.”

 Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim na imekwishatangulia.

[1] 74:04

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 26/05/2026