Ikiwa akiuliza ni njia gani bora ya kutafsiri Qur-aan, jibu ni kwamba njia sahihi zaidi ya kufasiri Qur-aan ni kufasiri Qur-aan kwa Qur-aan yenyewe. Kile kilichotajwa kwa jumla mahali fulani kimefafanuliwa mahali pengine, kile kilichofupishwa sehemu moja kimeelezewa kwa undani sehemu nyingine.

Ikiwa huwezi kupata maelezo ndani ya Qur-aan, basi rejea katika Sunnah, kwani Sunnah ndio inayoifafanua Qur-aan na kuiweka wazi. Imaam Abu ´Abdillaah Muhammad bin Idriys ash-Shaafi’iy amesema:

“Kila alichohukumuwa nacho Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kutokana na alivyofahamu katika Qur-aan.”

Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِتَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ بِمَا أَرَاكَ اللَّـهُ

”Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu kwa haki ili uhukumu kati ya watu kwa aliyokuonyesha Allaah.”[1]

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao na huenda wakapata kuzingatia.”[2]

وَمَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ إِلَّا لِتُبَيِّنَ لَهُمُ الَّذِي اخْتَلَفُوا فِيهِ ۙ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

”Hatukukuteremshia Kitabu isipokuwa ili uwabainishie yale waliyokhitilafiana kwayo na pia iwe ni mwongozo na rehema kwa watu wanaoamini.”[3]

Kwa ajili hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Zindukeni! Hakika nimepewa Qur-aan na mfano wake pamoja nayo.”[4]

Kwa maana ya Sunnah. Isitoshe ni kwamba Sunnah pia hushushwa kwake kwa njia ya wahy kama Qur-aan, ingawa haisomwi kama Qur-aan inavyosomwa. Imaam ash-Shaafi’iy na maimamu wengine wametoa dalili nyingi juu ya hili, ingawa hapa si mahali pa kueleza kwa undani. Madhumuni ni kwamba unapaswa kutafuta tafsiri ya Qur-aan kutoka ndani ya Qur-aan yenyewe. Ikiwa hutaipata, basi rejea ndani ya Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia Mu’aadh wakati alipomtuma kwenda Yemen:

“Utahukumu  kwa kitu gani?” Akasema: “Kwa Kitabu cha Allaah.” Akasema: “Usipopata?”
Akasema: “Kwa Sunnah ya Mtume wa Allaah.” Akasema: “Ikiwa hukupata?” Akasema: “Nitajitahidi kwa kutumia maoni yangu mwenyewe.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  akapiga kifua chake na kusema: “Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye ameongoza mjumbe wa Mtume wa Allaah kwenye yale yanayomridhisha Mtume wa Allaah.”[5]

Hadiyth hii imepokelewa ndani ya vitabu vya Sunan na vya Musnad kwa cheni ya wapokezi nzuri.

[1] 4:105

[2] 16:44

[3] 16:64

[4] Ahmad (4/130) na Abu Daawuud (4604). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Mishkaah” (163).

[5] Abu Daawuud (3592) na at-Tirmidhiy (1327), ambaye amesema kuwa cheni yake ya wapokezi haikuungana. Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan Abiy Daawuud” (3592).

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 84-86
  • Imechapishwa: 08/04/2025