La nne: Damu ya hedhi ikikatika kisha ikarejea katika ada basi inahesabika bila ya shaka kuwa ni damu ya hedhi. Mfano wa hilo ada ya mwanamke ni kwa siku nane. Baada ya siku nne damu yake ikakatika kwa siku mbili na halafu siku ya saba na ya nane ikarudi tena. Damu hii iliyorudi ni hedhi pasina shaka yoyote na kutathibiti hukumu za hedhi.

Ama kuhusu nifasi, damu ikikatika kabla ya siku arubaini kisha ikarudi tena ndani ya siku arubaini, damu hii itazingatiwa ni yenye kutia shaka. Kwa hivyo itakuwa ni wajibu kwa mwanamke kuswali na kufunga faradhi kwa wakati wake na ni haramu kwake kufanya yale ambayo ni haramu kwa mwanamke mwenye hedhi mbali na mambo ya wajibu. Baada ya kutwaharika atalipa zile ´ibaadah alizofanya katika kipindi cha damu hii yenye kutia shaka kama jinsi ni wajibu kwa mwanamke mwenye hedhi kulipa yale yaliyompita. Haya ndio maoni yanayojulikana kwa wanachuoni wa Hanaabilah.

Hata hivyo kauli sahihi ni kuwa maadamu damu inatoka katika kipindi cha nifasi inahesabika kuwa ni nifasi. Vinginevyo ni damu ya hedhi. Damu ikiendelea kutoka pasina kukatika inahesabika kuwa ni damu ya ugonjwa. Haya yanashabihiana na yale Ibn Qudaamah aliyotaja katika “al-Mughniy”[1] kutoka kwa Imaam Maalik ambaye amesema:

“Akipata damu siku mbili au tatu baada ya kuwa imekatika, inahesabika kuwa ni nifasi. Vinginevyo ni damu ya hedhi.”

Maoni haya ndio muqtadha wa chaguo la Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah. Uhakika wa mambo ni kuwa hakuna damu yenye kutia mashaka. Mambo yote yako wazi wazi kwa kutegemea ujuzi na uelewa wa watu. Qur-aan na Sunnah imebainisha kila kitu. Allaah (Subhaanah) hakumuwajibishia yeyote kufunga mara mbili au kufanya Twawaaf mara mbili ikiwa matendo hayo hayakufanywa kimakosa na hapo yakahitajia kurudiliwa. Pindi mja anapofanya kiasi na anavyoweza basi ameitakasa dhimma yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah Hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake.” (02:286)

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

“Basi mcheni Allaah muwezavyo.” (64:16)

[1] al-Mughniy (1/349).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article
  • Imechapishwa: 30/10/2016