Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mlango wa sita

Uwajibu wa kujifunza elimu

Ukishajua hilo na ukajua ya kwamba ni lazima wawepo maadui ambao wamekaa katika njia ya Allaah (Ta´ala), ni watu wenye ufaswaha, elimu na hoja mbalimbali. Basi hivyo ni wajibu kwako kujifunza dini ya Allaah kile ambacho itakuwa ni silaha yako upambane na hawa mashaytwaan ambao kasema kiongozi wao kumwambia Mola Wako (´Azza wa Jall):

فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ ۖ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ

“Basi kwa kuwa Umenihukumu kupotoka, nitawakalia [waja Wako] katika njia Yako iliyonyooka, kisha nitawaendea mbele yao na nyuma na kuliani kwao na kushotoni kwao; na wala Hutopata wengi wao wenye kushukuru.” (07:16-17)

MAELEZO

Ukishatambua haya ya kwamba maadui hawa wana ufaswaha, elimu na hoja mbalimbali wanazozivisha haki batili,  basi itakulazimu wewe kujiandaa kwa ajili yao. Kujiandaa huku kunakuwa namna mbili:

1 – Kile ambacho mtunzi (Rahimahu Allaah) anakiashiria, nacho ni wewe kuwa na hoja za Kishari´ah na za kiakili zitazoponda hoja mbalimbali na batili ya watu hawa.

2 – Uwe na ujuzi juu ya batili yao ili uweze kuwaraddi watu hawa. Kwa ajil hii ndio maana Shaykh-ul-Islaam (Rahimahu Allaah) amesema katika kitabu chake “Dar´ Ta´aarudhw-in-Naql wal-´Aql:

“Hakuna mtu anayekuja na hoja ili kufikia batili, isipokuwa hoja hiyo huwa dhidi yake na si upande wake.”

Jambo hili ni kama alivyosema Shaykh (Rahimahu Allaah). Mtu wa batili akija na dalili sahihi il kufikia batili yake, basi inakuwa ni hoja dhidi yake na upande wake. Ndio maana inatakiwa kwa yule ambaye anataka kuwajadili watu hawa, ahakikishe kwa kuzingatia mambo mawili:

1 – Aelewe ni elimu ipi walionayo ili aweze kuwaraddi kwayo.

2 – Azielewe dalili za Kishari´ah na za kiakili ili aweze kuwaraddi kwazo watu hawa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 49