Isitoshe “Allaah (Subhaanah) amesema ya kuwa Amewabainishia waja Wake ubainifu wa hali ya juu kabisa. Akamwamuru Mtume wake kubainisha na akaeleza ya kwamba amemteremshia Kitabu chake ili aweze kuwabainishia watu. Kwa hiyo az-Zuhriy akasema:

“Ujumbe ni wenye kutoka kwa Allaah, ni juu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kufikisha na ni juu yetu kujisalimisha.”

Kwa hivyo ubainifu huu ambao Yeye (Subhaanah) amejibebesha na akamwamrisha nao Mtume Wake, ima iwe makusudio ni kubainisha yale matamshi peke yake au maana peke yake au matamshi na maana vyote viwili. Wala haiwezekani ikawa kwamba makusudio ni kubainisha matamshi pekee pasi na maana, kwa sababu jambo hilo halina faida na hakufikiwi lengo la Ujumbe. Haiwezekani vilevile ikawa kumekusudiwa kubainisha maana pekee pasi na majulisho yake. Kwa hiyo pasi na shaka yoyote ikatambulika kuwa makusudio ni kubainisha matamshi na maana. Allaah (Ta’ala) ameteremsha Kitabu Chake – matamshi na maana zake – na akamtuma Mtume Wake ili kubainisha matamshi na maana zake. Kama ambavyo tunayakinisha na kusema kwa kukata kabisa ya kwamba amebainisha matamshi basi vivyo hivyo tunayakinisha na kusema kwa kukata kabisa ya kwamba amebainisha maana pia. Bali uhakika wa mambo ni kwamba kule kutilia kwake bidii katika kubainisha maana kulikuwa kukubwa zaidi kuliko kutilia kwake bidii katika kubainisha matamshi. Hivyo ndivo inavyotakikana, kwa sababu kubainisha maana ndio malengo na matamshi njia ya kuyafikia malengo hayo. Ni vipi basi angelitilia bidii zaidi njia kuliko anavyotilia bidii malengo? Ni vipi basi tutayakinisha ubainifu wake wa njia lakini tusiyakinishe ubainifu wake wa malengo? Si kuna jambo jengine hapa kama sio kutowezekana wazi wazi kabisa? Kama ingewezekana kwake kutobainisha makusudio ya yale matamshi ya Qur-aan basi ingeliwezekana pia kwake kutobainisha baadhi ya matamshi yake. Kama yangelikuwa makusudio yake si mengine isipokuwa kwenda kinyume na uhalisia wake, udhahiri wake na majulisho yake, na kwa ajili hiyo akawaficha nayo ummah na asiwabainishie nayo, basi hilo lingelikuwa ni tusi juu ya ujumbe na kule kukingwa kwake na kukosea. Isitoshe ingeliwafungulia njia mazanadiki na wapagani, katika Wakataaji na ndugu zao, kuyaficha baadhi ya yale yaliyoteremshwa kwake. Dhana kama hiyo inapingana na kule kumwamini yeye na kuamini ujumbe wake”[1].

[1] as-Swawaa´iq al-Mursalah (2/737-738) ya Ibn-ul-Qayyim.

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 46-48
  • Imechapishwa: 01/12/2025