Wanaopinga kuswali na viatu wana hoja tata ambazo zinahitaji kujadiliwa ili haki iweze kubainika. Licha ya kwamba sijawahi hata siku moja kumsikia mwanachuoni akitegemea hoja zao tata – jengine ni kwamba hoja tata za wajinga haziwezi kuwa dalili juu ya Shari´ah takasifu.

Hoja yao tata ya kwanza ni kwamba misikiti imepambwa na kuwekewa mazulia tofauti na hali ya misikiti wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Jawabu ya hoja hii ni kwamba kheri ipo katika yale aliyokuwa nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lau misikiti ingesalia kama ilivyokuwa katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi ingekuwa bora zaidi. Kuhusu kupamba na kuipendezesha misikiti, kumepokelewa makatazo juu ya jambo hilo. Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Qiyaamah hakitosimama mpaka watu wajifakhari kwa kupamba misikiti.”[1]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Sikuhamrishwa kujenga misikiti ya kifakhari[2].”

Ibn ´Abbaas amesema:

“Kwa hakika mtaipamba kama walivyofanya mayahudi na manaswara.”[3]

Wanaume wake ni wanaume wa Swahiyh – isipokuwa tu mwalimu wa Abu Muhammad bin as-Swabbaah bin Sufyaan, ambaye ni mkweli.

as-Swan´aaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

”al-Mahdiy amefanya vizuri pale aliposema katika ”al-Bahr”: ”Mapambo ya msikiti wa Makkah na Madiyanah haikuwa kutokana na maoni ya watu wa elimu wala kunyamaza kwao kuwa ni kuridhia. Bali ni matendo ya watawala wenye nguvu bila ridhaa ya wanazuoni. Waislamu wakanyamaza pasi na kuridhia.”[4]

[1] Abu Daawuud (449), Ibn Maajah (739), ad-Daarimiy (1/327), Ahmad (3/134-145, 152, 230 na 283) na Ibn Hibbaan. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (449). al-Munaawiy amesema katika “Faydhw-ul-Qadiyr”:

“Kwa maana kwamba watu watajifakhirisha juu ya usanifu wao, nakshi zao na michoro yao, kama wanavyojifakharisha watu wa Kitabu juu ya nyumba zao takatifu. Maoni mengine yanasema kwamba wanajifakharisha juu ya kuswali ndani yake, na si kwa majengo kama hayo.”

[2] Kwa maana ya kwamba, kwa mujibu wa al-Khattwaab, kujenga majengo marefu. Ibn-ul-Athiyr ametaja mfano wa hayo katika ”an-Nihaayah”  na kusema:

”Husemwa kwamba jengo ni la kifakhari ikiwa litapigwa lipu.”

[3] Abu Daawuud (448). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (448).

[4] Subul-us-Salaam (1/158).

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: as-Swalaah fiyn-Ni´aal, uk. 29-31
  • Imechapishwa: 23/06/2025