Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini Mizani siku ya Qiyaamah. Hadiyth inasema:

“Mja atapimwa siku ya Qiyaamah na hatokuwa na uzito sawa na ubawa wa mbu.”[1]

Matendo ya waja yatapimwa, kama ilivyotajwa kwenye mapokezi. Yanatakiwa kuaminiwa na kuthibitishwa. Mwenye kurudisha hilo anatakiwa kupuuzwa na asijadiliwe.

MAELEZO

Kuamini mizani siku ya Qiyaamah ni wajibu na ni moja katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Imetajwa katika Qur-aan na Sunnah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَالْوَزْنُ يَوْمَئِذٍ الْحَقُّ ۚ فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُم بِمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَظْلِمُونَ

“Kipimo kwa mizani siku hiyo itakuwa ni haki. Basi ambao mizani yao itakuwa nzito, hao ndio watakaofaulu na ambao mizani yao itakuwa khafifu, basi hao ni wale waliokhasirika nafsi zao kwa yale waliyokuwa wakizifanyia dhuluma Aayah Zetu.”[2]

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ

“Tutaweka mizani ya uadilifu siku ya Qiyaamah – hivyo nafsi haitodhulumiwa kitu chochote japo ikiwa uzito wa mbegu ya hardali Tutaileta. Inatosheleza Kwetu kuwa wenye kuhesabu.”[3]

Kumethibiti katika Sunnah ya kwamba matendo ya waja, madaftari ya kudhibiti na wao wenyewe vyote hivi vitapimwa. Kitachopimwa ni mambo matatu:

1- Mtendaji.

2- Matendo yake.

3- Madaftari yake ya kudhibiti.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ataletwa mtu mkubwa na mnene siku ya Qiyaamah. Hatokuwa na uzito mbele ya Allaah sawa na ubawa wa mbu. Someni:

فَلَا نُقِيمُ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَزْنًا

“Hatutowasimamishia siku ya Qiyaamah uzito wowote.”[4][5]

Wakati ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) alipopanda juu ya mti wa mbura wakashangazwa namna muundi wake ulivyo mwembamba ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Mnashangazwa na wembamba wa muundi wake? Ninaapa kwa Allaah kwamba ni yenye uzito zaidi kwenye mizani kuliko mlima wa Uhud.”[6]

Huu ni ushahidi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Swahabah huyu mtukufu. Hadiyth ni dalili vilevile inayoonyesha kuwa mtendaji atapimwa pamoja na daftari lake la kudhibiti na matendo yake. ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Siku ya Qiyaamah ataletwa mwanaume juu ya vichwa vya viumbe na aonyeshwe madaftari tisini na tisa [yaliyojaa madhambi]. Kila daftari [limejaa madhambi kwa] umbali wa kikomo cha macho. Aambiwe: “Unapinga chochote katika haya? Je, wahifadhi Wangu walikudhulumu?” Aseme: “Hapana, Mola wangu.” Kusemwe: “Hivi una udhuru au una tendo jema lolote?” Mtu huyo atanyamaza na aseme: “Hapana, Mola wangu.” Aambiwe: “Ndo, una tendo jema kwetu. Haudhulumiwi.” Halafu kutatolewa kadi iliyoandikwa ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake` iwekwe kwenye kitanga kimoja cha mzani. Atasema: “Ee Mola! Vipi kadi hii na madaftari yote haya?” Aambiwe: “Hutodhulumiwa.” Halafu kutawekwa yale madaftari kwenye kitanga kimoja cha mzani na ile kadi kwenye kitanga kingine cha mzani ambapo ile kadi itayashinda uzito yale madaftari.”[7]

[1] al-Bukhaariy (4729) na Muslim (2785).

[2] 07:8-9

[3] 21:47

[4] 18:105

[5] al-Bukhaariy (4729) na Muslim (2785).

[6] Ahmad (3991) na Ibn Hibbaan (7069). Ahmad Shaakir amesema: ”Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.” al-Albaaniy ameitaja katika ”as-Silsilah as-Swahiyhah” (2750) na (3192).

[7] Ahmad (2/213), at-Tirmidhiy (2639), Ibn Maajah (4300), Ibn Hibbaan (2523) na al-Haakim (1/6). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 81-82
  • Imechapishwa: 14/10/2019