251. Ni matendo yepi bora anayofanyiwa maiti?

Swali 251: Ni matendo yepi bora anayofanyiwa maiti? Ni ipi maana ya maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Katika kuwatendea wema wazazi baada ya kufa kwao ni wewe kuwaswalia wakati wa kuswali kwako na kuwafungia wakati wa kufunga kwao.”[1]?

Jibu: Bora wanachoweza kufanyiwa maiti ni kuwaombea du´aa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mwanadamu basi matendo yake hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika nayo au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”[2]

Kuwaombea du´aa maiti ni bora kuliko kila kitu; ni bora kuliko kuwaswalia, kuwatolea swadaqah, kuwahijia au kuwafanyia ´Umrah. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”… au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”

katika mtiririko wa matendo. Ingelikuwa matendo yamewekwa katika Shari´ah kumfanyia maiti basi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angelisema “au mtoto mwema mwenye kumtolea swadaqah, mwenye kumfungia na kadhalika”. Wakati alipotaja du´aa basi ikatambulika kuwa kuwaombea du´aa ndio bora zaidi kuliko kumpa maiti zawadi ya matendo mema.

Kuhusu Hadiyth, neno “swalah” kunamaanishwa kuwaombea du´aa. Swalah (الصلاة) inakuja wakati mwingine ikiwa na maana ya du´aa. Allaah (Ta´ala) amesema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ ۖ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

”Chukua katika mali zao swadaqah uwatwaharishe na uwatakase kwazona na uwaombee duaa; hakika duaa yako ni utulivu kwao. Allaah Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.”[3]

[1] al-Muswannaf (3/387) kupitia kwa Ibn Abiy Shaybah.

[2] Muslim (1631).

[3] 09:103

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/276)
  • Imechapishwa: 11/02/2026