Hadiyth hii inafahamisha mambo mawili:

1 – Siku za Tashriyq ni siku za kula, kunywa, kuonesha furaha na bashasha na kupanua neema kwa familia na watoto kwa yale wanayoyapata ya kupumzika mwili na kustarehe nafsi kwa yale yasiyokuwa haramu wala si kizuizi kwa utiifu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Siku ya ´Arafah, siku ya Nahr na siku za Tashriyq ni sikukuu yetu sisi waislamu.”[1]

Hakuna ubaya wowote wa kujitanua katika kula na kunywa, khaswa nyama, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alizielezea kuwa ni siku za kula na kunywa maadamu haifiki kiwango cha israfu na ubadhirifu au kudharau neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

2 – Siku hizi ni siku za kumtaja Allaah (´Azza wa Jall). Hilo ni kwa kuleta Takbiyr baada ya kila swalah na katika nyakati zote na hali zote zinazofaa kwa kumtaja Allaah (´Azza wa Jall). Miongoni mwa hilo ni kumtaja Allaah wakati wa kula na kunywa, kwa namna ya kutaja jina la Allaah mwanzoni na kumsifu mwisho – hata kama hili ni la jumla kwa nyakati zote – lakini linasisitizwa zaidi ndani ya siku hizi.

[1] Ahmad (4/152), Abu Daawuud (2419), at-Tirmidhiy (773), an-Nasaa’i (5/252) na wengineo. at-Tirmidhiy amesema:

”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

Ni Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Khuzaymah (2100) na Ibn Hibban (8/368).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdullaah bin Swaalih al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahaadiyth ´Ashrah Dhil-Hijjah wa Ayaam-it-Tashriyq, uk. 41-42
  • Imechapishwa: 15/05/2025