25. Mfumo wa wakanushaji juu ya sifa za Allaah

Wakanushaji wamekubaliana juu ya kuthibitisha sifa za Allaah zinazoafikiana na akili zao na kupinga zile ambazo haziafikiani na akili zao. Haya ni mamoja ziwe zinaafikiana na Qur-aan na Sunnah au zisiafikiane. Kwa mujibu wao ni akili ndio yenye kuamua Allaah atathibitishiwa au kukanushiwa sifa zipi.

Baada ya hapo wakatofautiana yale ambayo akili haiwezi kuyathibitisha wala kuyakanusha. Wengi wao wakakanusha hilo na kuonelea kuwa ni majazi. Wengine wakalinyamazia hili na wakaegemeza suala hili kwa Allaah wakati huohuo wakakubaliana juu ya kwamba haziashirii dalili yoyote. Wanadai eti kwa kutumia mfumo huu wanaoanisha kati ya dalili za kiakili na za Qur-aan na Sunnah. Wamesema uongo. Dalili za kiakili na za Qur-aan na Sunnah zinakubaliana juu ya kumthibitishia Allaah sifa kamilifu. Hakuna sifa zozote zilizotajwa katika Qur-aan na Sunnah zinazopingana na akili japokuwa akili inaweza kutoelewa ukina wake. Wakanushaji hawa wanakumbushia kuhusu wale ambao Allaah amesema juu yao:

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُواْ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُواْ إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُواْ أَن يَكْفُرُواْ بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلاَلاً بَعِيدًا وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْاْ إِلَى مَا أَنزَلَ اللّهُ وَإِلَى الرَّسُولِ رَأَيْتَ الْمُنَافِقِينَ يَصُدُّونَ عَنكَ صُدُودًا فَكَيْفَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ ثُمَّ جَآؤُوكَ يَحْلِفُونَ بِاللّهِ إِنْ أَرَدْنَا إِلاَّ إِحْسَانًا وَتَوْفِيقًا

“Je, huwaoni wale wanaodai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako na yale yaliyoteremshwa kabla yako, namna ambavyo wanataka wahukumiane kwa hukumu za kishaytwaan na hali wameamrishwa wakanushe hiyo? Na shaytwaan anataka awapoteze upotofu wa mbali. Na wanapoambiwa: “Njooni kwenye yale aliyoyateremsha Allaah na kwa Mtume”, utawaona wanafiki wanakugeukilia mbali kwa mkengeuko. Basi itakuwaje utakapowafika msiba kwa sababu ya yale iliyotanguliza mikono yao, kisha wakakujia wakiapa: “Hatukutaka isipokuwa mazuri na mapatano”.”[1]

Wanafanana na watu hawa kwa njia zifuatazo:

1- Makundi yote mawili yanadai kwamba yanaamini yale aliyoteremshiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ingawa hawaamini yale yote aliyokuja nayo.

2- Pindi wakanushaji hawa wanapoitwa katika kuthibitisha sifa kamilifu za Allaah zilizothibiti katika Qur-aan na Sunnah, wanakengeuka na kukataa. Hali kadhalika wale wanafiki pindi wanapoitwa katika kuamini yale aliyoteremshiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanakengeuka.

3- Wakanushaji hawa wana mashaytwaan ambao wanawafuata kichwa mchunga na wanawatanguliza mbele ya yale waliyokuja nayo Mitume. Wakati wa kutofautiana wanataka wahukumiwe nao si kuhukumiana kwa Qur-aan na Sunnah. Vivyo hivyo wale wanafiki wanataka wahukumiane na hukumu za kishaytwaan pamoja na kuwa wameamrishwa kuzikufuru.

4- Wakanushaji hawa wanadai kwamba hawakutaka kwa mfumo huu isipokuwa jambo zuri la kuoanisha kati ya akili na Wahy. Hali kadhalika ndivyo walivyoapa wale wanafiki.

Kila mwongo anayejificha nyuma ya batili zake na kujidhihirisha kwa haki, basi huja kwa madai batili ambayo kwayo anaeneza batili zake. Lakini yule ambaye Allaah anamtunukia elimu, uelewa, hekima na nia nzuri, hatumbukii katika batili na wala hapelekwi na madai batilifu.

[1] 04:60-62

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 69-70
  • Imechapishwa: 07/05/2020