25. Kumebainishwa adabu za chooni lakini si ´Aqiydah?

Haiwezekani kabisa ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amepewa jukumu la kufikisha awe eti hakuwabainishia watu maudhui hayo. Nadharia hiyo ni kumtuhumu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufanya khiyana na kuficha elimu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewabainishia watu kila wanayoyahitaji katika mambo ya dini yao, na khaswa jambo la ´Aqiydah ambayo ndio msingi. Hakufa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa baada ya Allaah kuikamilisha dini kupitia kwake na kuyaweka mambo yote wazi. Kitendo cha baadhi ya watu kutoyajua haya si hoja. Ubainifu upo. Mapungufu yako kwake yeye, na si kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ikiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewabainishia watu kila kitu katika mambo ya dini yao mpaka adabu za kukidhi haja; ni vipi basi asiwafunze ´Aqiydah? Ni vipi basi asiwafunze maana ya majina na sifa za Allaah? Ni kwa nini hakusema kuwa hazitakiwi kufahamika kama zilivyokuja kutoka kwa Allaah? Ni kwa nini hakuwabainishia watu jambo hilo na badala yake watu kama al-Jahm bin Swafwaan na Waaswil bin ´Atwaa wao ndio wakalazimika kuwabainishia watu? Ni jambo lisilowezekana kabisa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 53
  • Imechapishwa: 30/07/2024