Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) analingania kwa Allaah na katika dini Yake kwa utambuzi, kwa sababu ni lazima mlinganizi awe anajua kile anacholingania kwacho. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amesimama ´Arafah katika hajj ya Kuaga Allaah alimteremshia:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.”[1]

Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameshuhudia kuwa dini hii imekamilika. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakufa isipokuwa baada ya Allaah kuikamilisha dini kupitia kwake. Kwa hivyo yule anayekuja na nyongeza zisizofaa na kuziingiza ndani ya dini na kuwapambia watu maana yake ni kuwa anaituhumu dini hii kuwa haikukamilika na kwamba inahitaji kuongezewa kitu kisichomo ndani ya Qur-aan na Sunnah. Kufanya hivo ni kumkadhibisha Allaah (´Azza wa Jall) aliyesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ

”Leo nimekukamilishieni dini yenu… ”

Kile ambacho hakikuwa ni dini wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi hakiwezi kuwa dini baada ya kufa kwake. Baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuna nyongeza au kuzua kitu katika dini. Dini haihitaji nyongeza. Nyongeza zote ni shari, Bid´ah na upotofu na sio katika dini. Haijalishi kitu hata kama wazushi na wapotofu watawapambia nayo watu, sisi hatujali. Tunatosheka na Qur-aan na Sunnah, kwa sababu Allaah ameikamilisha dini kabla ya kufa kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama alivosema Imaam Maalik (Rahimahu Allaah).

[1] 5:3

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 51-52
  • Imechapishwa: 30/07/2024