25. Fikiria mtu mchangamfu mbele ya mfalme

Mfano wa mtu anayegeuka katika swalah yake kwa macho au kwa moyo wake ni kama mfano wa mtu ambaye ameitwa na mfalme. Wakati aliposimamishwa mbele yake na mfalme huyo akaanza kumwita na kuzungumza naye, huku yeye katika kipindi hicho anageuka kutoka kwa mfalme kulia na kushoto na moyo wake umegeukia mbali na mfalme huyo kiasi kwamba haelewi anamsemeza, kwa sababu moyo wake haupo hapo mbele ya mfalme. Je, mtu huyu atadhani nini kwamba mfalme atamfanyia? Je, si angalau daraja ya chini zaidi anayostahiki ni kuondolewa kutoka mbele ya mfalme akiwa amechukiwa, amesukumwa mbali na ameshuka thamani machoni mwake? Basi swalah ya mtu huyu haiwezi kuwa sawa na swalah ya yule ambaye moyo wake uko mbele ya Allaah katika swalah yake ambaye moyo wake umejaa utukufu wa Yule aliyesimama mbele Yake na shingo yake imevunjika kwa unyenyekevu na anahisi haya kwa Mola wake (Ta´ala) kugeukia kwa asiye Yeye au kumgeukia Yeye mwenyewe. Hassaan ´Atwiyyah amesema kuhusu swalah ya watu hawa wawili:

”Hakika watu wawili huweza kuwa katika swalah moja, lakini tofauti ya fadhilah baina yao ni kama baina ya mbingu na ardhi.”

Hiyo ni kwa kuwa mmoja wao moyo wake umeelekea kwa Allaah (´Azza wa Jall) na mwingine ni mwenye kusahau na mwenye kupumbaa. Basi iwapo mja atamwelekea kiumbe kama yeye mwenyewe na baina yao kuna pazia, hilo halihesabiwi kama kuelekea wala kukaribia. Je, vipi basi hali itakuwaje kwa Muumba (´Azza wa Jall)? Iwapo atamwelekea Muumba (´Azza wa Jall), lakini baina yake na Muumba wake kuna pazia la matamanio, wasiwasi na nafsi yake imejaa kupendezwa nayo, basi vipi hilo litaitwa kuelekea wakati tayari wasiwasi na mawazo yamempa msongamano na kumpeleka kila upande?

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 44-45
  • Imechapishwa: 05/08/2025