25. Bid´ah – sababu kubwa ya makinzano

Lengo hapa ni kuangazia chanzo cha tofauti katika tafsiri. Miongoni mwa sababu zake kubwa zaidi ni Bid´ah batili zilizowasukuma wenye nazo kuyapotosha maneno kutoka mahali pake stahiki na wakafasiri kwazo maneno ya Allah na Mtume wake (Swalla Allahu Alayhi Wasallam) kinyume na maana yake halisi na kuyatafsiri kwa maana zisizo sahihi. Miongoni mwa misingi ya elimu juu ya hili ni kwamba mtu anapaswa kutambua ni maoni yepi wanayopinga, kwamba ndiyo haki, atambue kuwa tafsiri ya Salaf inapingana na tafsiri yao na atambue kuwa tafsiri yao ni mpya na iliyozuliwa. Kisha mtu anapaswa kujua, kwa msaada wa Allaah wa kuweza kuibainisha haki, kwa elimu ya kina upotovu wa tafsiri yao. Haya yamewatokea pia wale waliokuja baadaye ambao wameandika vitabu vinavyozitolea Hadiyth maelezo na kuzitafsiri.

Kuhusu wale wanaokosea katika dalili na si katika kile wanachokitolea dalili, ni kama vile makundi mengi ya Suufiyyah, watoa mawaidha, wanazuoni wa Fiqh na wengineo, wanaifasiri Qur-aan kwa maana sahihi pasi na Qur-aan kujulisha juu ya mambo hayo. Mfano ni kama yale ambayo anatumbukia ndani yake mara nyingi Abu ´Abdir-Rahmaan as-Sulamiy katika “Haqaa-iq-ut-Tafsiyr”. Hata hivyo endapo wangelifasiri kwa maana batili, wao pia wamejumuishwa katika kipengele cha kwanza, nako ni kule kukosea katika dalili na kile kinachotolewa dalili. Kwa sababu inakuwa mbovu ile maana waliyoikusudia.

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 82-83
  • Imechapishwa: 07/04/2025