247. Je, inafaa kumpa maiti thawabu za kisomo changu cha Qur-aan?

Swali 247: Je, inafaa kumpa maiti thawabu za kisomo cha Qur-aan katika Ramadhaan na pia kumfanyia Twawaaf?

Jibu: Hapana neno. Mtu akitaka kuswali, kutoa swadaqah, kuhiji, kusoma Qur-aan au kufunga na baadaye kumjaalia thawabu zake maiti hapana vibaya. Imepokelewa katika Hadiyth Swahiyh ya kuwa bwana mmoja alimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema:

“Mama yangu amekufa. Nafikiri kuwa endapo angeliweza kuzungumza basi angelitoa swadaqah. Je, anapata ujira ikiwa nitamtolea swadaqah?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ndio.”[1]

Jengine ni kwamba alimpa idhini Sa´d bin ´Ubaadah (Radhiya Allaahu ´anh) kumtolea swadaqah mama yake. Swadaqah nyenginezo ni kama ´ibaadah zingine, kwa vile hakuna tofauti baina yake.

Hakujapokelewa chochote kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kinachokataza mtu kumtolea swadaqah maiti mpaka tuseme kuwa tunakomeka kwa yale yaliyopokelewa. Wakati Sunnah inapotaja aina fulani ya ´ibaadah basi ´ibaadah nyenginezo zinapata hukumu hiyohiyo kama zilizotajwa. Hilo khaswa kwa kuzingatia kwamba hayakusemwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), bali baadaye imekuwa ni suala katika hali maalum. Fatwa yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba inafaa kwa mtu kumtolea swadaqah mama yake haina maana kuwa yasiyokuwa hayo yamekatazwa.

Hata hivyo ninachoona ni kuwa mtu ayajaalie matendo mema kwa ajili ya nafsi yake na awaombee du´aa wazazi wake waliokwishatangulia mbele ya haki. Kuwaombea du´aa ndio bora kuliko kuwatolea swadaqah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mwanadamu basi matendo yake hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika nayo au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”[2]

Hakusema “au mtoto mwema anayemfanyia ´ibaadah”. Kujengea juu ya hilo ni kwamba kuwaombea du´aa wazazi wako ni bora zaidi kuliko kuwapa zawadi ya swalah, kisomo chako cha Qur-aan au ´ibaadah nyenginezo. Yafanye matendo kwa ajili ya nafsi yako. Hivo ndivo alivyoelekeza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (2670) na Muslim (1004).

[2] Muslim (1631).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/253-254)
  • Imechapishwa: 10/02/2026