245. Je, inafaa kwa mtu kuswali swalah ya Sunnah na matendo mengine kama hayo kwa ajili ya baba yake aliyekufa?

Swali 245: Je, inafaa kwa mtu kuswali swalah ya Sunnah na matendo mengine kama hayo kwa ajili ya baba yake aliyekufa?

Jibu: Ndio. Inafaa kwa mtu kumswalia swalah za Sunnah baba yake au waislamu wengine. Inafaa pia kumtolea swadaqah. Hakuna tofauti kati ya swadaqah, swalah, swawm, hajj na ´ibaadah nyenginezo. Lakini mambo haya yamewekwa katika Shari´ah au ni mambo yanayofaa tu? Haya ni mambo yanayofaa na hayakuwekwa katika Shari´ah. Jambo lililowekwa katika Shari´ah kwa mtoto ni yeye kumuombea du´aa baba yake. Isipokuwa ikiwa ni mambo yaliyofaradhishwa, katika hali hiyo atamfanyia nayo baba yake kama inavyofahamisha Sunnah. Mfano wa hilo ni kama baba amekufa na anadaiwa swawm ya faradhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote mwenye kufa na juu yake yuko na swawm, basi afungiwe na walii wake.”[1]

Hilo linakusanya funga hiyo imefaradhishwa na Shari´ah, kama vile swawm ya Ramadhaan,  au swawm ambayo mtu amejizalimisha mwenyewe, kama vile swawm ya nadhiri.

Sio katika mambo yaliyowekwa katika Shari´ah kutoa zawadi ya ´ibaadah au thawabu kuwapa jamaa; bali ni jambo linalofaa peke yake. Kilichowekwa katika Shari´ah ni kuwaombea du´aa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mwanadamu basi matendo yake hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika nayo au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”[2]

Amesema “mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa”,  hakusema “mtoto mwema anayemswalia, anayemfungia ua anayemtolea swadaqah. Hilo likafahamisha jambo bora ambalo mtoto anayeweza kuwafanyia wazazi wake baada ya kuaga kwao dunia ni kuwaombea du´aa.

Pengine mtu akasema kuwa hafahamu ni vipi jambo litakuwa lenye kujuzu na lisiwe limewekwa katika Shari´ah. Mambo ni hivyo. Ni jambo linalofaa, lakini halikuwekwa katika Shari´ah. Ni jambo linalojuzu kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amelijuzisha. Bwana mmoja alimjilia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema:

“Mama yangu amekufa. Nafikiri kuwa endapo angeliweza kuzungumza basi angelitoa swadaqah. Je, anapata ujira ikiwa nitamtolea swadaqah?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ndio.”[3]

Vivyo hivyo Sa´d bin ´Ubaadah (Radhiya Allaahu ´anh) alimtolea mama yake swadaqah ya shamba lake, ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkubalia[4]. Hata hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwaamrisha ummah wake kuyafanya matendo hayo kwa njia ya kuwa kama Shari´ah kwao. Bali alichofanya ni yeye kuwapa idhini kwa wale wanaotaka kufanya mambo hayo. Mfano wa hayo ambapo kitendo kinaweza kuwa kinafaa na wakati huohuo kisiwe chenye kuwekwa katika Shari´ah ni kisa cha yule bwana ambaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwagiza katika kikosi. Kila alipokuwa akiwaswalisha wenzake akawa anamalizia kwa kusoma Suurah “al-Ikhlaasw”. Waliporejea wakamweleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kitendo cha bwana huyo. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Muulizeni ni kwa nini alikuwa anafanya hivo.” Bwana yule akasema: “Hakika mambo yalivyo ni kwamba ni sifa za Mwingi wa huruma na kwa ajili hiyo mimi nikapenda kuisoma.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mwelezeni kuwa Allaah anampenda.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkubalia kitendo chake hicho. Kwa hiyo ni kitendo kinachofaa lakini hakikuwekwa katika Shari´ah. Hata hivyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakukiweka katika Shari´ah. Kwa ajili hiyo yeye mwenyewe hakuwa akimalizia swalah kwa Suurah “al-Ikhlaasw” na wala hakuwaamrisha ummah wake kufanya hivo. Kwa hivyo ikafahamisha kuwa yapo matendo ambayo inafaa kuyafanya lakini hata hivyo hayakuwekwa katika Shari´ah. Kwa maana nyingine ni kwamba mtu akiyafanya hatokaripiwa lakini hata hivyo hatotakwa kuyafanya.

[1] al-Bukhaariy (1952) na Muslim (1147).

[2] Muslim (1631).

[3] al-Bukhaariy (2670) na Muslim (1004).

[4] al-Bukhaariy (2756).

[5] al-Bukhaariy (7375) na Muslim (813).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/250-252)
  • Imechapishwa: 09/02/2026