240. Je, baba analipwa thawabu kwa pesa ambayo mtoto anamtolea kutoka katika pesa zake mwenyewe?

Swali 240: Je, baba analipwa thawabu kwa pesa ambayo mtoto anamtolea kutoka katika pesa zake mwenyewe?

Jibu: Maoni sahihi ni kwamba thawabu zake zinamfikia. Imethibiti kwamba bwana mmoja alimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema:

“Mama yangu amekufa. Nafikiri kuwa endapo angeliweza kuzungumza basi angelitoa swadaqah. Je, anapata ujira ikiwa nitamtolea swadaqah?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ndio.”[1]

Jengine ni kwamba Sa´d bin ´Ubaadah (Radhiya Allaahu ´anh) alimuuliza kama anaweza kulitoa swadaqah shamba lake kwa ajili ya mama yake ambaye kishakufa, ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akampa idhini.

Hata hivyo bora ni yeye kujitolea swadaqah mwenyewe na wazazi wake awaombee du´aa. Hivyo ndivo alivyotuelekeza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Anapofariki mwanadamu basi matendo yake hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika nayo au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”[2]

Amesema “au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa“ na hajasema amtolee swadaqah au amtendee matendo mema, ingawa mtiririko umetaja matendo.

[1] al-Bukhaariy (2670) na Muslim (1004).

[2] Muslim (1631).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/246)
  • Imechapishwa: 04/02/2026